22.1 C
New York

Vijana Afrika wanavyotumika vita vya Urusi, Ukraine

Published:

YOUNDE, Cameroon

CAMEROON inatajwa kuwa moja ya nchi zinazotoa vijana wengi walioko vitani kulisaidia jeshi la Urusi dhidi ya Ukraine. Mbaya zaidi, vijana hao hawaendi kwa kupenda.

Kwa mujibu wa taarifa, hupelekwa Urusi kwa ahadi za kupewa ajira nzuri na uraia wa nchi hiyo ya Ulaya Mashariki, lakini ghafla hujikuta wakipewa silaha na kuwekwa mstari wa mbele katika vita.

Kufikia Mei, 2026, mamlaka za Ukraine zilieleza kuwa raia takribani 3,000 wa nchi za Afrika, ikiwamo Cameroon, wameingizwa kwenye jeshi la Urusi kupigana na Ukraine.

Mbali na Cameroon, nchi zingine za Afrika zilizotajwa kuongoza kwa raia wake kutumiwa na Urusi ni Ghana, Misri, Kenya na Uganda. Serikali ya Kenya inakiri kuwa raia wake zaidi ya 200 wamekimbilia Urusi kuanzia Januari, 2026, lakini ni 18 pekee alioweza kurudi.

Aprili, 2026, Serikali ya Cameroon nayo ilitoa taarifa kuwa Urusi imeripoti vifo 16 vya raia wa Taifa hilo la Afrika Mashariki na saba kati yao walikuwa vitani nchini Ukraine.

Hata hivyo, idadi inayoripotiwa ni ndogo, ukilinganishwa na uhalisia, kwa mujibu wa mwandishi wa DW, Dorcas Ekupe. Amesema: “Ukitazama machapisho na uhalisia uliopo, familia zinazolilia wapendwa wao, idadi hiyo ni ndogo.”

Kwa upande mwingine, Ekupe na hata wachambuzi wa siasa wanakubaliana kuwa sababu kubwa ya vijana wa Cameroon na nchi zingine za Afrika kuvutika kwenda Urusi na hatimaye kujikuta vitani ni umasikini.

“Wengi walikwenda Urusi wakiamini kwamba wangepata kazi nzuri katika sekta za ujenzi au ulinzi, na wapo waliokwenda wakidhani wangeingia kwenye programu za masomo. Wanapofika Urusi, walijikuta wakiishia kwenye uwanja wa vita.”

Hata hivyo, sheria za kimataifa hazizuii mtu kujitolea kuisaidia nchi nyingine kwenye vita, ingawa hiyo haitoi nafasi kwa njia mbaya za kuajiri kutumika, ikiwamo kulazimishwa kwa vitisho, rushwa na biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.

Aidha, sheria za kimataifa zinaweka wazi kuwa endapo raia wa kigeni atafia vitani, nchi aliyokuwa akiisaidia haitowajibika kwa lolote. Itakuwa ni hasara yake na familia.

Kwa sasa Serikali ya Cameroon imeendelea kuwaonya raia wake, hasa vijana, kujihusisha na migogoro ya nje, ikiwamo vita kati ya nchi jirani za Urusi na Ukraine.

Lakini, kwa wachambuzi wa siasa, onyo pekee halitoshi, na badala yake Serikali ya Cameroon na zingine za Afrika zinapaswa kufanya jitihada kubwa za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa ajira kwa vijana.

Pia, kama ilivyofanya Ghana, Serikali za Afrika zinapaswa kutuma ujumbe kwa Urusi, kwamba inapaswa kuacha mara moja mfumo wa kuwatumia raia wake kwenye vita, kwa mujibu wa wachambuzi.

Related articles

Recent articles