LOS ANGELES, Marekani
LEJENDARI wa muziki wa Soul na R&B nchini Marekani, Lionel Richie, alikimbizwa hospitali wikiendi iliyopita, kisha kuwekwa ‘ICU’ mjini St. Louis.
Richie (77), ambaye aliwahi kutamba kupitia ngoma zake nyingi, zikiwamo ‘Hello’ na ‘All Night Long’, alipelekwa hospitali baada ya shoo yake ya Jumamosi mjini Forest Park.
Kwa mujibu wa chanzo kilichohojiwa na mtandao maarufu wa habari za mastaa, Richie aliomba kiti wakati shoo ikiendelea, hali iliyomaanisha kuwa hakuwa sawa kiafya.
Hii inakuwa mara ya pili kwa Richie kulazwa baaada ya Juni, 2026, ambapo alipelekwa hospitali baada ya shoo yake katika Ukumbi wa Grand Casino mjini St. Paul. Alirejea wiki moja baadaye na kuendelea na Tamasha la ‘Earth, Wind & Fire’.
Alizaliwa Juni 20, 1949 huko Tuskegee, Alabama, na jina lake halisi ni Lionel Brockman Richie Jr. Mbali ya kuimba, pia ni mwandishi wa nyimbo, prodyuza na mtangazaji wa vipindi vya televisheni.
Ni mtoto wa Lionel Brockman Richie, mwanajeshi wa zamani wa Marekani aliyehudumu katika kitengo cha mifumo. Mama yake Richie, Alberta R. Foster, alikuwa mwalimu.
Hata hivyo, tayari damu ya muziki ilishachomoza kwenye familia kupitia kwa bibi yake wa upande wa baba, Adelaide Mary Brown, ambaye alikuwa mpigaji kinanda mzuri.
Kwa upande wake, Richie baada ya kumaliza sekondari, alijiunga na Chuo cha Tuskegee, ambako alisomeshwa kwa ufadhili baada ya kuonesha kiwango kizuri katika mchezo wa tenesi.
Hatimaye, Richie alihitimu elimu ya juu akiwa na Shahada (Digrii) ya Sayansi ya Uchumi ikiwa pia na masomo ya Uhasibu.
Lakini, kwa kipindi chote hicho, ndoto yake ilikuwa ni kuwa mchungaji, hasa katika Kanisa la Episcopal alikobatizwa. Aliachana na ndoto hiyo baada ya kuona haendani na mienendo ya uchungaji, hivyo akaamua kujitosa moja kwa moja kwenye muziki.
Baada ya miaka mingi ya ‘kujitafuta’, Richie alianza kupata umaarufu katika miaka ya 1970 akiwa mwandishi na mwimbaji wa iliyokuwa bendi kubwa wakati huo, Commodores.
Ni baada ya kutoa ngoma ‘Easy’, ‘Sail On’, ‘Three Times a Lady’ na ‘Still’, kabla ya kuacha na bendi hiyo. Mwaka 1980, si tu aliandika, bali pia ndiye aliyekuwa prodyuza wa wimbo ‘Lady’ wa mkongwe Kenny Rogers, ambao ulioshika namba moja katika chati za Billboard Hot 100.
Mwaka uliofuata, aliandika na akawa prodyuza wa ‘Endless Love’, wimbo alioimba na Diana Ross na hadi sasa uko kwenye orodha ya zile 20 zilizowahi kuuza nakala nyingi duniani.
Pia, ndiyo wimbo mkubwa zaidi kwa kila mmoja wao. Tangu hapo, Richie ameachia ngoma nyingi zilizofanya vizuri, zikiwamo ‘You Are’, ‘My Love’, ‘Truly’ na ‘Say You, Say Me’.
Mbali na kuwa mmoja ya wanamuziki wenye mauzo makubwa katika historia, pia Richie amebeba tuzo nne za Grammy, zikiwamo za Wimbo Bora wa Mwaka (We Are the World) na Albamu Bora ya Mwaka (Can’t Slow Down).
Kwa nyakati tofauti, Richie aliwahi kufika Afrika na kufanya shoo katika nchi za Morocco, Misri na Libya. Alikuwa mkosoaji mkubwa wa hatua ya Marekani kuivamia Iraq na wakati fulani alisema angetamani siku moja kufanya shoo katika nchi hiyo ya Kiarabu.
Katika maisha binafsi, Richie kwa sasa hana mke lakini aliwahi kuoa mara mbili. Alianza na mpenzi wake wa chuo, Brenda Harvey, ambapo walifunga ndoa mwaka 1975.
Waliachana mwaka 1993 na Richie kumuoa Diane Alexander miaka miwili tu baadaye. Katika ndoa yake na Diane, alipata watoto wawili; wa kiume aitwaye Miles Richie na bibiye Sofia, kabla ya kuachana mwaka 2004.


