20.4 C
New York

Maajabu ya kulala wikiendi kwa afya yako

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KULALA kwa saa moja au mbili za ziada katika siku za mapumziko ya wiki (wikiendi) kunapunguza hatari ya kupata shinikizo la damu, utafiti umebaini.

Katika hatua nyingine, wataalamu wameenda mbali zaidi wakishauri kuwa ni vizuri kiafya kutokubalisha muda wako wa kulala na kuamka.

Utafiti huo wa Chama cha Wataalamu wa magonjwa ya moyo cha Ulaya na umeanikwa katika Mkutano wake wa mwaka uliofanyika mjini Munich, Ujerumani.

Ni utafiti uliofanyika kwa miaka saba (2016 – 2023) na kuhusisha sampuli ya watu wazima 40,727 nchini Korea ya Kusini.

Katika utafiti huo, watu hao waliulizwa utaratibu wao wa kulala, kwa maana ya muda wanaotumia, katika siku za wikiendi, ukilinganisha na siku za kawaida.

Majibu ya utafiti yalionesha kuwa wale waliojiongezea dakika 60 au 120 za kulala wikiendi walipunguza hadi asilimia tisa uwezekano wa kupata shinikizo la juu la damu.

Akieleza zaidi, Nawon Lee kutoka Chuo Kikuu cha Korea mjini Seoul ameeleza kuwa kukosa usingizi wa kutosha si tu kunachochea msongo wa mawazo, bali pia kunasababisha mishipa ya damu kufanya kazi kwa kasi, hivyo kuongeza shinikizo la damu.

Kwa takwimu za sasa, kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), asilimia 33 ya watu bilioni 1.4 wenye umri kati ya miaka 30 hadi 79 duniani wanakabiliwa na tatizo hilo.

Wakati huo huo, takwimu za WHO zinaleza kuwa kwa sasa shinikizo la juu ya damu ni moja ya vyanzo vikuu vya vifo vya mapema duniani.

Related articles

Recent articles