Na Hassan Mwasha, Gazetini
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ana siku 14, kwa mujibu wa Ibara ya 50(4) ya Katiba, kuteua Makamu wa Rais baada ya Dk. Emmanuel Nchimbi kujiuzulu wadhifa huo jana Agosti 25, 2026.
Aidha, uwepo wa wanasiasa wengi wenye uwezo na uzoefu ndani ya Serikali na Chama chake (CCM) inaweza kumfanya Rais Dk. Samia apitie wakati mgumu kuchagua mtu wa kumpa nafasi hiyo.
NANI KUVAA VIATU VYA DK. NCHIMBI?
Ni swali linalopaswa kupatiwa majibu siku ndani ya wiki mbili (mwisho ni Septemba 18, 2026). Miongoni mwa wenye sifa na uwezo wa kukalia kiti cha Dkt. Nchimbi ndani ya Serikali ya sasa ni Dk. Mwigulu Lameck Nchemba. Uzoefu wake serikalini si wa kutilia shaka.
Kwa nyakati tofauti, Dk. Nchemba ambaye ni mtaalamu wa uchumi kitaaluma, aliwahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali, zikiwamo za Waziri wa Fedha, Waziri wa Mambo ya Ndani, na sasa Waziri Mkuu.
Ukiweka kando jina lake, pia Rais Dk. Samia anayo nafasi ya kumgeukia mkongwe mwingine, George Simbachawene. Nafasi kubwa aliyoshika hivi karibuni ni Waziri wa Mambo ya Ndani. Alipotolewa hapo, Patrobas Katambi alipewa kijiti hicho.
Wakati huo huo, uzoefu na utendaji kazi wa Doto Biteko nao unampa nafasi ya kuingia kwenye orodha ya wanaoweza kuaminiwa na Rais Dk. Samia kurithi mikoba ya Dk. Nchimbi.
Achilia mbali nafasi nyingine mbalimbali, Biteko aliwahi pia kuwa Naibu Waziri Mkuu, hivyo si tu ni mwanasiasa mwenye uwezo, bali pia amebeba uzoefu wa kutosha kushika nafasi nyeti ya Makamu wa Rais.
UTATA KUJIZULU KWA DK. NCHIMBI
“Nimejiridisha pasipo na shaka kuwa mheshimiwa Rais anataka mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu.” Hiyo ni kauli ya Dkt. Nchimbi katika taarifa yake aliyoisambaza mitandaoni.
Kwa mujibu wake, ni ahadi aliyompa Rais Dk. Samia wakati anamteua, kwamba angeondoka iwapo angeona anahitajika Makamu mwingine.
Hata hivyo, kauli yake hiyo imeonekana kuzua mjadala mzito mitandaoni, wengi wakikosa majibu ya swali hili; ni mabadiliko yapi hayo yasiyohitaji kasi, uwezo na uzoefu wa Dkt. Nchimbi?
Kwa upande mwingine, wapo waliohusisha kujiuzulu kwake na kauli ‘tata’ aliyoitoa wiki chache zilizopita, alipodai kuwa wananchi wanapaswa ‘kuipigania’ Katiba Mpya.
Kama itakumbukwa, kauli yake hiyo ilizua hisia mseto, ambapo wakosoaji wake wa ndani na nje ya Chama walihisi amechagua kujitenga na mwelekeo wa Serikali iliyoko madarakani.


