Na Hassan Mwasha, Gazetini
HISTORA inaweza kuzitaja skendo za ufisadi za ESCROW na RICHMOND kama nyakati mbaya zaidi katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Dk. Jakaya Kikwete. Wakosoaji wake wamekuwa wakishikilia hapo.
Skendo za ufisadi zilizoibuka wakati huo na kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa, kutangaza kujizulu, hatua iliyotafsiriwa kuwa ni kubeba ‘msalaba’ wa wengine ili maisha yaendelee.
Hata hivyo, wakosoaji wake hawajawahi kusahau na wanakiri mara zote kwamba kama kuna kipindi Bunge limewahi kuwa na msisimko mkubwa na kufuatiliwa zaidi na wananchi, basi ni miaka 10 ya uongozi wa Dk. Kikwete.
Bunge lililokuwa na idadi nzuri ya wanasiasa wa upinzani na hoja za moto, ambazo moja ya matokeo yake chanya katika kuibana Serikali ni kuibuliwa kwa skendo za ufisadi zilizomsukuma Lowassa kujiuzulu.
Nje ya Bunge, wanasiasa wa upinzani walikuwa uhuru mkubwa. Huenda zilikuwepo changamoto za hapa na pale lakini kwa kiasi kikubwa Dk. Kikwete alimudu kuvaa ‘ngozi ya chuma’ kuvumilia kejeli, matusi na kila aina ya presha kutoka kwa wapinzani.
Kwa upande wake, siasa haukuwa uwanja wa vita. Siasa haikuwa uadui. Kwa kuwapa nafasi ya kuzungumza kile walichojisikia, aliweza kusikiliza na kuokota mawili au matatu ya kusaidia kuimarisha utendaji wa Serikali yake.
Kinyume chake, endapo Dk. Kikwete asingeruhusu uwanja mpana ule kwa siasa za upinzani, angekuwa amejinyima mwenyewe kioo cha kujitazama na kuona madhaifu yake katika kuiongoza nchi. Aligundua hilo, akawaachia kipaza sauti, kisha akawa msikilizaji mzuri na kujibu kwa staha pale alipoona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Tutoke huko. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliwahi kuwa na Freeman Mbowe. Licha ya kazi kubwa aliyoifanya akiwa Mwenyekiti (sasa Mstaafu), wapo wanaomuona na hata kumwita ‘dalali’, kwamba ni mtu wa CCM na Serikali.
Kwanini? Ni kutokana na aina ya siasa zake. Kwa Mbowe, kama ilivyokuwa kwa Kikwete, hakuwa muumini mkubwa wa siasa za ‘jino kwa jino’. Na badala yake, aliamini katika demokrasia na mazungumzo.
Kwa wengine, huenda ingekuwa ngumu kukubali kwenda Ikulu baada ya kusota gerezani kwa miezi nane kwa kesi ya ugaidi. Mbowe alifanya tutofauti. Alikwenda na kukaa meza moja na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Ni muumini wa mazungumzo.
Mbaya kwake, hizo siyo aina ya siasa wanazovutiwa nazo wafuasi na hata baadhi ya viongozi wa upinzani na wako sahihi katika mtazamo wao huo. Kwamba siasa za upinzani si kusifia na kupiga makofi. Kazi hiyo inatosha kufanywa na Chama tawala au watumishi wa umma.
Iko hivi; lengo kuu la chama cha upinzani si tu Tanzania, bali hata duniani kote, ni kutafuta na kuibua madhaifu ya Serikali iliyoko madarakani ili kuwashawishi wananchi kuwa kinastahili kupewa nafasi ya kushika dola.
Hivyo, chama cha upinzani kinachoamua kujisogeza na kujenga ‘urafiki’ wa karibu na Serikali kitakuwa kimejimaliza chenyewe kwani kitapoteza uwezo wa kukosoa kwa ‘sauti kubwa’ kama wafanyavyo sasa akina John Heche. Siasa zitapoteza mvuto!
Nikimaanisha, licha ya siasa kuhitaji ‘mafundi’ wa demokrasia aina ya Kikwete na Mbowe, pia ubora wake unahitaji uwepo wa ‘wakorofi’ wenye uthubutu wa aina ya Heche (Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA). Wanaoweza kuifanya Serikali isilale, ijitathimini na kujisahihisha wakati wote.
Ni kama alivyonufaika mzee Kikwete, ambaye Serikali yake ilipata nafasi ya kuwa macho wakati wote na kujisahihisha kupitia hoja nzito za wanasiasa wa upinzani, wakiwamo Tundu Lissu, Moses Machali, Halima Mdee, Julius Mtatiro, na James Mbatia.
Naomba kuwasilisha …


