Na mwandishi wetu, Gazetini
SIKU tatu tu baada ya mwanafunzi mwenye umri wa miaka 14 kuua wenzake nane kwa kuwamiminia risasi, lilitokea tukio jingine lenye sura hiyo nchini Thailand.
Chalong Riewrang, mwanasiasa wa zamani mwenye umri wa miaka 71, alifika ofisini kwa rafiki kwa kile kilichoelezwa kuwa alikwenda kumdai pesa zake.
Mazungumzo na Thongchai Yenprasert yaliishia vibaya na hatimaye Chalong kumpiga risasi rafiki yake huyo, ambaye alifariki hapo baadaye.
Chalong aliondoka eneo la tukio na kisha kumpigia simu mwandishi wa habari anayefahamiana naye, akimsimulia kile kilichotokea.
Hata baada ya kukamatwa na polisi, hakuwa na wasiwasi na badala yake alisema dereva wa rafiki yake ndiye aliyeanza kuchomoa bastola wakati wa ugomvi wao.
Tukio jingine lilitokea mjini Prachinburi, Mashariki mwa Bangkok, ambako mtumishi wa jeshi la polisi alimuua kwa kumtwanga risasi mkewe baada ya ugomvi uliotokea wakiwa kwenye gari. Polisi huyo naye alijiua kwa kujipiga risasi ya kichwa.
Hiyo ni mifano michache kati ya matukio mengi ya mauaji yanayohusisha matumizi ya bastola nchini Thailand. Idadi ya vifo vya aina hiyo ni kati ya 2,000 hadi 3,000 kila mwaka.
Takwimu zinaonesha kuwa Thailand ina bastola zaidi ya milioni 10 zinazomilikiwa na raia, huku milioni nne kati ya hizo zikimilikiwa kinyume cha sheria. Uholela huo unakuja, licha ya kwamba zipo sheria na taratibu zinazodhibiti umiliki wa silaha.
Mathalan, ili kununua, lazima upate kibali cha ununuzi. Hata baada ya kununua, lazima upate kibali cha umiliki. Kubeba silaha yako nje ya nyumba, lazima pia uwe na kibali.
Kwa upande mwingine, kununua silaha kutoka nje ni gharama, hivyo wengi kati ya raia huzipata kwa kuuziwa kwa njia za panya.
Hata hivyo, wengi wanaona kuna changamoto katika sheria za kudhibiti silaha. Mathalan, kigezo cha afya ya akili hazipewi umuhimu kwa mtu kupewa kibali cha kumiliki.
Pili, hakuna ufuatiliaji unaofanywa na mamlaka kujua namna silaha inavyohifadhiwa nyumbani kwa mmiliki. Mfano, kijana aliyeua wenzake aliichukua bastola ya babu yake.
Bunduki zaidi ya 200,000 huingia Thailand kila mwaka na maofisa wa polisi na watumishi wengine wa vyombo vya dola wamekuwa wakizipata kwa bei ya chini.
Lakini, kwa kuwa sheria zinaruhusu kuziuza baada ya miaka mitano ya umiliki, wamekuwa wakipata fedha nyingine kupitia biashara hiyo.


