24.3 C
New York

Dk. Mwigulu atoa siku 14 kituo cha Oparesheni kuanza kazi

Published:

Na Faraja Mulungu, Gazetini

WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, ametoa siku 14 kwa wizara na taasisi zote zinazohusika na Kituo cha Kitaifa cha Pamoja cha Oparesheni kupeleka wawakilishi wake ili kituo hicho kianze kufanya kazi mara moja, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha usalama wa mipaka ya bahari na kulinda uchumi wa bluu.

Akizungumza leo Julai 31, 2026 katika hafla ya kupokea na kuzindua boti mbili za doria aina ya PB Sailfish 02 na PB Sailfish 03 zilizofanyika Bandarini Dar es Salaam, Dk. Mwigulu alisema wizara na taasisi husika zinapaswa kutekeleza agizo hilo ndani ya muda alioweka ili kituo hicho kianze kutoa matokeo yaliyokusudiwa.

“Wizara na taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa majukumu katika Kituo cha Kitaifa cha Pamoja cha Oparesheni zipeleke wawakilishi wote wanaohitajika ndani ya siku 14 kuanzia leo. Kituo hiki kianze kazi mara moja ili kuleta tija inayokusudiwa,” amesema Dk. Mwigulu.

Aidha, amezitaka Wizara zinazoshughulikia masuala ya Muungano kuimarisha ushirikiano ili kuziba mianya yote inayoweza kutumiwa na wahalifu katika mipaka ya mwambao wa bahari.

Katika kuhakikisha boti hizo zinafanya kazi ipasavyo, Waziri Mkuu aliziagiza taasisi zote zinazozitumia kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya mafuta, matengenezo na shughuli za doria, akisisitiza kuwa ukosefu wa bajeti usije ukazuia matumizi ya vifaa vilivyonunuliwa kwa gharama kubwa.

“Nimekuwa nikiona vifaa muhimu vikishindwa kutoa huduma kwa sababu ya ukosefu wa fedha za uendeshaji. Hili linapingana na dhamira ya Serikali ya kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema.

Boti hizo mbili zimenunuliwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 1.6 na zinatarajiwa kuimarisha doria, uchunguzi na mapambano dhidi ya uhalifu baharini pamoja na kulinda rasilimali za uchumi wa bluu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, alisema jina Sailfish linatokana na samaki aina ya Sulisuli, anayefahamika kwa kasi yake kubwa baharini, akisema boti hizo zinaashiria uwezo mpya wa Serikali katika kuimarisha usalama wa maeneo ya pwani.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Rhimo Nyansaho amesema ujio wa boti hizo unaongeza uwezo wa Taifa katika kulinda mipaka ya bahari kwa kutumia mifumo ya kisasa, huku Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Jim Yonazi, akiahidi kusimamia matumizi yake kwa ufanisi. “Upande wetu tutaendelea kutekeleza kazi zetu kwa uaminifu mkubwa,” amesema Dk. Yonaz.

Related articles

Recent articles