LONDON, Uingereza
KAMA ilivyo kawaida, katika kila msimu mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL), huwa kuna timu tatu zilizopanda daraja. Safari hii (2026-27), ni Coventry City, Hull City na Ipswich Town.
Je, zitakaza na kufanya maajabu EPL msimu ujao wa 2026-27 au zitarudi zilikotoka, kwa maana ya Daraja la Kwanza (Championship)?
COVENTRY CITY
Coventry ‘Sky Blues’ ni moja ya klabu zilizoasisi Ligi hiyo na imerejea kwa mara ya kwanza tangu iliposhuka daraja miaka 25 iliyopita.
Baada ya kufika hadi Daraja la Pili, Coventry walipambana na hatimaye kurejea EPL wakiwa mabingwa wa Championship (Daraja la Kwanza) msimu uliopita (2025-26).
Wako chini ya kocha wa zamani wa Chelsea, Frank Lampard, na wameimarisha kikosi kwa kuwanasa Loum Tchaouna na Aurele Amenda waliovunja rekodi ya usajili klabuni hapo.
Pia, straika wao tegemeo ni raia wa Marekani, Haji Wright, ambaye ameshafunga mabao 45 katika misimu mitatu ya hivi karibuni.
HULL CITY
Si wageni wa EPL lakini misimu tisa ya hivi karibuni waliitumia wakiwa Championship. Hull City wamerudi EPL kwa ‘playoff’ waliyocheza Mei, 2026.
Sergej Jakirovic amebaki kwenye benchi la ufundi baada ya kutwaa tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka wa Championship msimu uliopita (2026-27).
Jakirovic raia wa Bosnia, ameboresha kikosi chake kwa ajili ya EPL kwa kuwasajili Matt Targett na Hidemasa Morita lakini dili kubwa zaidi ni la kipa wa zamani wa timu ya Taifa ya England, Jack Butland aliyetokea Rangers ya Scotland.
IPSWICH TOWN
Kama ilivyo kwa Coventry, Ipswich nayo ilikuwa sehemu ya timu zilizoasisi Ligi Kuu ya England. Walishuka daraja msimu wa 2024-25 na sasa wamerejea.
Ipswich ‘Tractor Boys’ walikata tiketi ya kucheza EPL baada ya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Championship msimu uliopita (2025-26).
Aliyefanikisha mpango ni kocha Gary O’Neil, ambaye aliwahi kuzinoa Bournemouth na Wolves, kabla ya kwenda Strasbourg baada ya kocha Liam Rosenior kutimkia Chelsea.
O’Neil aliyechukua nafasi ya Kieran McKenna, ameimarisha safu ya ushambuliaji ya Ipswich kwa ajili ya EPL kwa kuwanasa Emersonn, Abdul Fatawu na Daizen Maeda.
Wakati huo huo, kocha huyo ameboresha ‘ukuta’ kwa kumnasa beki aliyecheza Kombe la Dunia mwaka huu (2026) akiwa na timu ya Taifa ya Morocco, Issa Diop.


