29.4 C
New York

Mjukuu wa Idi Amin na ndoto za ‘kuiteka’ dunia

Published:

KAMPALA, Uganda

NDOTO kubwa aliyonayo Aziz Abdul, ambaye ni mjukuu wa Rais wa zamani wa Uganda, Idi Amin, ni kuiteka dunia kupitia mchezo wa ngumi. Anapigana uzito wa juu.

Aziz alikuwa ukingoni jana Julai 29, 2026 mjini Glasgow, Scotland, ambapo alimvaa Damar Thomas wa Uingereza katika pambano la michuano ya Jumuhiya ya Madola.

Lakini, bondia huyo mwenye umri wa miaka 25 alipoteza na kumtupia lawama mwamuzi, licha ya ukweli kwamba alicheza faulo nyingi, ikiwamo kumpiga kichwa mpinzani wake.

Hata hivyo, hata baada ya kung’oka kwenye mashindano, bado ndoto yake haijaota mbawa, akiamini ipo siku ataiteka dunia kupitia uwezo wake ulingoni.

Kwa upande mwingine, Aziz anayeishi Uganda hakuwahi kumuona babu yake, Idi Amin, ingawa naye aliwahi kuwa bondia, kabla ya kujitosa kwenye siasa na baadaye kuwa Rais wa Uganda.

Wakati Idi Amin akiwa dikteta nchini Uganda hadi alipokombilia uhamishoni baada ya utawala wake kuangushwa mwaka 1978, Aziz alikuwa mdogo.

Historia inakumbusha; Idi Amin aliingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 1971 na kuiendesha Uganda kwa ‘mkono wa chuma’ kwa miaka nane.

Chini ya utawala wake, yaliripotiwa matukio ya watu wanapatao 500,000 kuuawa, huku raia wa kigeni kutoka Asia wakilazimishwa kuondoka.

Vyanzo mbalimbali vya habari vinadai kuwa alioa mara sita na kupata watoto takribani 60 hadi anapoteza maisha mwaka 2003 akiwa uhamishoni Saudi Arabia.

Katika maisha ya ngumi, kabla ya kuwa mwanasiasa, Idi Amin aliwahi kushikilia ubingwa wa uzito wa light-heavy kwa miaka tisa nchini Uganda.

Je, Aziz anayeishi Kampala anamzungumziaje babu yake huyo? Na je, anajisikiaje anapoitwa mjukuu wa dikteta? Anajibu hilo kwa kusema:

“Kuna wanaomzungumzia kwa mazuri na wapo wanaosema mabaya yake. Ndiyo maana huwa sipendi kumzungumzia. Sidhani kama ni vizuri kuzungumzia mabaya ya mtu ambaye hayupo.”

Related articles

Recent articles