23.5 C
New York

Megawati 2,115 za Bwawa la Nyerere mbioni, Tanesco yatoa ratiba

Published:

Na Faraja Mulungu, Gazetini

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kuwa ujenzi wa njia mpya ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma umefikia asilimia 94, hatua inayokaribisha kukamilika kwa miundombinu muhimu itakayobeba umeme unaozalishwa na Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.

Kutokana na hatua za mwisho za ujenzi huo, Tanesco imetangaza kuwa kutakuwa na katizo la muda la huduma ya umeme katika baadhi ya mikoa nchini ili kutoa nafasi ya kukamilisha kazi za kiufundi zinazohitajika kabla ya njia hiyo kuanza kutumika kikamilifu.

Akizungumza Julai 28, 2026 mkoani Pwani, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle, amesema katizo hilo litafanyika kwa awamu mbili, kuanzia Julai 30 hadi Agosti 4, na baadaye Agosti 11 hadi 17, 2026, kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni katika siku na maeneo yatakayopangwa.

Amefafanua kuwa kazi hizo zinahusisha kuvusha nyaya za umeme katika eneo la Mkambarani, mkoani Morogoro, kwa kuzingatia viwango vya usalama kwa wafanyakazi, wananchi na miundombinu mingine.

“Hakutakuwa na ukosefu wa umeme kwa siku zote mfululizo. Huduma itasitishwa kwa nyakati tofauti kulingana na ratiba ya maeneo husika ambayo wananchi wataendelea kufahamishwa,” amesema Gowele.

Kwa mujibu wa Tanesco, mradi huo wa njia ya umeme wa kilovolti 400 una urefu wa kilomita 345 na unatekelezwa kwa ufadhili wa asilimia 100 wa Serikali ya Tanzania kwa gharama ya takribani Sh bilioni 514.

Meneja wa Mradi huo, Mhandisi Newton Mwakifwamba, alisema kukamilika kwa njia hiyo kutakuwa hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa taifa wa usafirishaji wa umeme kwa kuongeza uwezo wa kusafirisha nishati inayozalishwa katika Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle.

“Mradi huu utaongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, kuboresha uthabiti wa gridi ya taifa na kuiwezesha Tanzania kushiriki kwa ufanisi zaidi katika biashara ya umeme ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ukanda wa Kusini mwa Afrika,” amesema Mwakifamba.

Ameongeza kuwa njia hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya nishati ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya umeme kwa wananchi, viwanda na shughuli nyingine za uzalishaji, sambamba na kuongeza uwezo wa kuuza umeme kwa nchi jirani kupitia miradi ya kikanda ya kuunganisha mifumo ya umeme.

Tanesco imewahakikishia wananchi kuwa maandalizi yote yamefanyika ili kupunguza athari za katizo hilo na kwamba huduma itarejeshwa mara moja baada ya kukamilika kwa kazi katika kila eneo.

Aidha, shirika hilo limebainisha kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara haitaguswa na ratiba hiyo ya katizo, huku likiwaomba wananchi wa maeneo yatakayoathirika kuwa wavumilivu kwa kuwa maboresho hayo yanalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.

Related articles

Recent articles