Na mwandishi wetu, Gazetini
SERIKALI kupitia Wizara ya Madini imekamata dhahabu yenye uzito wa gramu 4,402.20 na thamani ya zaidi ya Sh bilioni 1.2 katika eneo la Kiluvya, Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya operesheni zinazoendelea za kudhibiti utoroshaji wa madini na kulinda mapato ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumatatu, Julai 27, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesemasema dhahabu hiyo ilikamatwa Julai 25, 2026 na vyombo vya dola baada ya kubainika kuwa ilikuwa ikisafirishwa kinyume cha taratibu za kisheria za biashara ya madini.
Amesema endapo mzigo huo ungefanikiwa kutoroshwa, Serikali ingepoteza mapato ya Sh 108,365,127 yaliyopaswa kulipwa kupitia mrabaha (Royalty), ada ya ukaguzi, Response HIV Levy, Service Levy na Withholding Tax.
“Dhahabu hii kwa sasa imehifadhiwa salama katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ikiwa imefungwa kwa lakiri za Tume ya Madini namba MC 1066128 na MC 1066129, huku uchunguzi ukiendelea dhidi ya watuhumiwa waliokamatwa,” amesema Mavunde.
Waziri huyo amesema Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini kwa kupanua masoko na vituo rasmi vya ununuzi wa madini ili kuwapa wachimbaji na wafanyabiashara fursa ya kuuza madini yao kwa njia halali, yenye uwazi na inayoongeza mapato ya Serikali.
Aidha, alionya kuwa mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na usafirishaji au biashara ya madini nje ya mfumo rasmi atachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Pamoja na Serikali kupunguza baadhi ya kodi na tozo ili kurahisisha biashara ya madini, bado kuna watu wachache wanaoendelea kutorosha madini kwa tamaa ya kupata faida kubwa kwa kukwepa sheria. Hilo halitavumiliwa,” amesema.
Mavunde pia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha uchunguzi ili kuwabaini na kuwafikisha mbele ya sheria watu wote wanaohusika katika mtandao wa utoroshaji wa madini, badala ya kuwakamata wasafirishaji pekee.
Amesisitiza kuwa lengo la Serikali ni kuvunja mitandao yote ya biashara haramu ya madini, akibainisha kuwa sekta ya madini imeendelea kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya mapato yasiyo ya kodi na mchango wake katika ukuaji wa uchumi unapaswa kulindwa.
Ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya utoroshaji wa madini, akieleza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, vyombo vya dola na wadau wa sekta ya madini ni muhimu katika kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha zinawanufaisha Watanzania wote.


