Na mwandishi wetu, Gazetini
SIYO habari mpya kwamba mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva, amejiunga na Newroz SC akitokea Al-Talaba, zote za Ligi Kuu nchini Iraq.
Huu ni msimu wa pili kwa Msuva akiwa Iraq, ikukumbukwa kuwa alitua kwa mara ya kwanza mwaka 2024 aliposajiliwa na Al-Najma.
Kwa sasa, maisha yake mapya yako Newroz SC, ambayo masikani yake ni mjini Kurdistan. Ilianzishwa mwaka 1994 na jina lake la utani ni ‘City’s Hope’ (Tumaini la Mji).
Newroz ilipanda daraja kuingia Ligi Kuu msimu wa 2020–21 baada ya kufungwa mechi moja tu kati ya 13 na kukusanya pointi 30.
Klabu hiyo inamiliki Uwanja wake wa nyumbani unaopokea mashabiki 14,500. Uwanja huo uliogharimu Dola milioni 12 ulianza kutumika Oktoba 26, 2024, kwa mchezo uliishuhudia Newroz ikishinda 2-1 dhidi ya Al-Najaf.
Hata hivyo, kwa miaka mitano ya ushiriki wake Ligi Kuu, mafanikio pekee kwao ni kushika nafasi ya pili msimu wa 2021-22.
Aidha, kwa miaka mitano ya hivi karibuni, benchi la ufundi la Newroz limekuwa la moto kiasi cha makocha kuingia na kutoka.
Iraq Wali Kareem aliajiriwa mwaka 2021 lakini aliondoka mwaka uliofuata. Nizar Mahrouz alichukua nafasi yake lakini naye alidumu kwa mwaka mmoja.
Baada ya wazawa hao, Newroz ilimpa ajira kocha raia wa Brazil, Jorvan Vieira, lakini naye hakuzidi mwaka mmoja. Nafasi yake akachukua kocha mzawa, Qahtan Chatir.
Qahtan, kama ilivyokuwa kwa wenzake, naye alifanya kazi mwaka mmoja, kabla ya kocha raia wa Sweden, Yasin Aras, kupewa mikoba yake.
Hata hivyo, Yassin alitia fora zaidi kwani alidumu miezi mitatu tu, ndipo alipoajiriwa kocha wa sasa, Wali Kareem, ambaye alianza kazi mwaka 2025.
Kwa ujumla, Msuva amefunga mabao 21 na kutoa asisti tisa katika michezo 63 alizocheza Ligi Kuu ya Iraq (Iraq Stars League).
Kabla ya kutimkia Iraq, Msuva alikuwa Ligi Kuu ya Saudi Arabia akiitumikia Al-Qadsiah ya Ligi Daraja la Kwanza, ambako alifunga mabao 11 katika michezo 43.
Klabu hiyo ilimsajili akitokea Ligi Kuu ya Morocco (Botola Pro), ambako huko alikipiga Difaa El Jadida na Wydad Casablanca.
Akiwa na vigogo hao kwa nyakati tofauti, Msuva alicheza mechi 116 za Ligi Kuu, akifunga mabao 38 na kutoa asisti 13.
Pia, kwa mujibu wa takwimu zake akiwa Morocco, alifunga mabao nane na asisti tatu katika mechi 28 za Ligi ya Mabingwa.
Msimu wa mafanikio zaidi ni ule wa 2021-22, ambapo Wydad ilitwaa taji la Ligi ya Mabingwa, pia ubingwa wa pili mfululizo wa Ligi Kuu.


