BOSTON, Marekani
KICHAPO cha mabao 2-1 kutoka kwa Hispania katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia kilihitimisha safari ya ‘kizazi cha dhahabu’ cha timu ya soka ya Taifa ya Ubelgiji kwenye michuano hiyo.
Thibaut Courtois, Romelu Lukaku, Kevin de Bruyne na Axel Witsel ndiyo wachezaji pekee waliokuwa wamebaki kwenye kikosi cha kizazi cha dhahabu.
Kizazi kile kilichokuwa na Eden Hazard, Mousa Dembele, Vincent Kompany, with Dries Mertens na Marouane Fellaini.
Kizazi ambacho kilifika robo fainali katika michuano ya mwaka huo (2014), kisha nusu fainali na mshindi wa tatu msimu uliofuata (2018).
Ikiwa na nyota hao waliokuwa kwenye ubora wao, Ublegiji ilifika mara mbili hatua ya robo fainali za EURO (2016 na 2020), kabla ya kuishia makundi katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022.
Kwa wakosoaji na hata wachambuzi wa soka barani Ulaya, ni Ubelgiji iliyopaswa kutwaa taji kubwa lolote, kama si Kombe la Dunia, basi hata EURO.
Baada ya kuambulia patupu mara zote hizo, ni wazi umri hautowaruhusu Courtois, Lukaku, De Bruyne na Witsel kurejea katika fainali zijazo za Kombe la Dunia mwaka 2030.
Hilo la umri linaweza pia kuonekana kwa mastaa wengine, wakiwamo Leandro Trossard (31), Brandon Mechele (33), Timothy Castagne (33), Hans Vanaken (33), na Thomas Meunier (34).
Hivyo, matarajio ya mashabiki wa soka la Ubelgiji yanahamia kwa vijana chipukizi, akiwamo straika Charles de Ketelaere.
Ketelaere (25), alionesha kiwango kizuri katika fainali za mwaka huu, ambapo alifunga mabao matatu na kutoa ‘asisti’ moja.
Pia, tegemeo lipo kwa nahodha wao, Youri Tielemans, ambaye ana umri wa miaka 29 na ndiye aliyesawazisha na kufunga bao la ushindi dhidi ya Senegal katika hatua ya 32 Bora.
Vilevile, nyota wawili wenye umri wa miaka 24 kila mmoja, Amadou Onana (Aston Villa) na Jeremy Doku (Manchester City), nao ni tumaini jipya la Ubelgiji ijayo.
“Chipukizi wanaweza kujifunza kwa kile kilichotokea,” amesema kiungo mkongwe, De Bruyne.


