26.6 C
New York

Miaka 30 ya Bongo Fleva ni zaidi ya ubunifu, burudani

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

UNAWEZA kufikiria kuhusu shoo nyingi za muziki zilizowahi kufanyika hapa nchini lakini ‘Miaka 30 ya Bongo Fleva’ imekuja na upekee mkubwa.

Ni shoo ya Julai 10, 2026, ikiwa na sura tofauti na ubunifu mkubwa ulioleta mvuto wa aina yake kwenye tasnia ya burudani.

Kuwakutanisha kwenye jukwaa moja wasanii waliowahi kufanya vizuri kwenye kiwanda cha Bongo Fleva ilileta ladha tofauti na kuchangamsha gemu.

Kwamba katika jukwaa moja, wapenzi wa muziki huo wa kizazi kipya walipata kuwasikia Dully Sykes, Mr. Blue, Mabaga Fresh, TMK Family, Afande Sele, Mr. Nice, Dudu Baya, Chid Benz, Mchizi Mox, Mwasiti, Stara Thomas, n.k.

Sura nyingine iliyoongeza mvuto wa shoo hiyo ya Miaka 30 ya Bongo Fleva ni kuhusisha wanamuziki wa nje waliowahi kutamba enzi hizo.

Wasanii ambao wakati akina Dully Sykes wanatamba, nao ngoma zao zilikuwa zikifanya vizuri katika vituo vya redio na runinga hapa nchini.

Kupita usiku wa Miaka 30 ya Bongo Fleva, walishuhudiwa Nyota Ndogo na Jua Cali wakiiwakilisha Kenya kwa shoo nzuri zilizowavutia mashabiki wao na wapenzi wa muziki kwa ujumla.

Ubunifu mwingine mzuri katika shoo hiyo ni asilimia kubwa ya wasanii kutumbuiza ‘live’, bila msaada wa ‘CD’ au ‘flash’. Nyota Ndogo alifanya kwa kiwango bora mno, kama ilivyo kwa wasanii wengi.

Hii si tu ilionesha maandalizi mazuri ya Miaka 30 ya Bongo Fleva, bali pia uwezo na ukomavu mkubwa wa kutumbuiza waliokuwa nao wasanii wa enzi hizo.

Pia, ni somo kubwa pia kwa wasanii wa kizazi cha sasa, kwamba ubora wa mwanamuziki hutegemea pia uwezo wake wa kutumbuiza kwa vyombo, badala ya kutegemea ‘CD’ au ‘flash’ awapo jukwaani.

Je, nini hatua inayofuata katika awamu ya pili? Shoo hiyo itakuja na upekee upi? Nini hatima ya wakongwe walioonekana jukwaani, ambao wengi wao ‘walishapotea’, Miaka 30 ya Bongo Fleva imewapa mzuka wa kurudi kwenye gemu?

Related articles

Recent articles