24.9 C
New York

Baadhi ya maneno Morogoro na Tanga kukosa umeme

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limetangaza kukatika kwa huduma ya umeme katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro na Tanga kuanzia Julai 9 hadi 14, 2026, kupisha utekelezaji wa kazi za uvutaji waya (stringing) katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma.

Kwa mujibu wa taarifa ya Tanesco, kazi hizo zinalenga kuwezesha ujenzi wa mradi huo mkubwa kuendelea kwa usalama na kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Umeme utakatika katika maeneo mbalimbali kila siku kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni, huku maeneo yatakayoathirika yakijumuisha Kiwanda cha Mkulazi kupitia Mkulazi Feeder pamoja na maeneo yanayohudumiwa na Turiani Feeder.

Maeneo mengine ni wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro, ikiwemo baadhi ya kata na vijiji vya Dakawa, Mvomero, Mkindo, Mtibwa, Dumila, Madudu na Mbigiri. Baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga na Gairo mkoani Morogoro pia vitaathirika.

Tanesco imesema hatua hiyo ni sehemu ya maandalizi muhimu ya kukamilisha Mradi wa Chalinze–Dodoma, unaolenga kuimarisha uwezo wa kusafirisha umeme nchini. Shirika hilo limeomba radhi kwa usumbufu utakaotokea na kuwataka wananchi kutogusa waya wowote wa umeme uliokatika au kuanguka chini. Wananchi wametakiwa kutoa taarifa kupitia namba ya huduma kwa wateja 180.

Related articles

Recent articles