34.9 C
New York

Dube na hadithi ya maumivu iliyofikia tamati Yanga

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

HIVI karibuni, Yanga iliachana na mshambuliaji wake raia wa Zimbabwe, Prince Dube, ambaye amejiunga na Hardrock ya Ligi Kuu nchini humo. Amerudi nyumbani.

Kwamba nyota huyo amehitimisha safari ya miaka sita ya kucheza Ligi Kuu Bara, tangu aliposajiliwa na Azam mwaka 2020 akitokea Highlanders ya Zimbabwe.

Dube alijiunga na Yanga wakati wa usajili wa dirisha kubwa kuelekea msimu wa 2024-25 akitokea kwa matajiri wa Chamazi, Azam.

Hata hivyo, kwa sehemu kubwa ya maisha yake ndani ya Yanga, hakufanikiwa kucheza katika sura ya mchezaji wa daraja lake.

Ni kweli alimaliza msimu wake wa kwanza akiwa na mabao 13 kwenye Ligi lakini hakuwa Dube yule waliyemuota Wanayanga baada ya kutangaziwa usajili wake.

‘Ukatili’ wake mbele ya lango ulipungua kwa kiasi kikubwa, wakati mwingine akiigharimu timu kwa kukosa nafasi nyingi za wazi.

Wakati fulani, akiwa kwenye anguko la kiwango chake, ziliibuka taarifa kuwa ameomba asicheze moja ya mechi, hiyo ikithibitisha kuwa alipoteza kabisa hali ya kujiamini.

Kama haijasahaulika, kuporomoka kwa kiwango chake wakati huo kulimuibua hata straika wa zamani wa Yanga, David Molinga ‘Falcao’, aliyemsapoti kwa kumpa moyo.

Hata hivyo, kwa wakati wote huo, mashabiki na wanachama hawakuwahi kumkatia tamaa – walisimama naye na kumshangilia kwa nguvu, na wakati mwingine kila alipogusa mpira.

Ni wakati ambao wangeweza kumzomea, kumtolea lugha chafu, na hata kutaka asipewe nafasi ya kuingia kikosini. Walichagua kusimama naye.

Katika ujumbe wake wa kuaga, Dube amekiri hilo, kwamba kuna wakati hakustahili heshima na sapoti aliyopewa. Amesema:

“Nikiitazama klabu hii, nawaona watu walioniamini, walionipenda, walioona mwanga ndani yangu katika kipindi ambacho sikustahili.

“Nawaona watu ambao walikuwa upande wangu wakati dunia ikiwa imenikataa. Wakati wengine walipoona nimefeli, nyinyi (mashabiki wa Yanga) mliona bado nina kitu ndani yangu.”

Ujumbe huo unaweza kuthibitisha kwamba Dube angetamani kubaki Yanga endapo angekuwa kwenye ubora aliowahi kuwa nao akiwa na ‘uzi’ wa Azam.

Amemaliza msimu akiwa na mabao 10 kwenye Ligi. Mbaya zaidi, Yanga inakabiliwa na presha kubwa ya kukifanyia ‘upasuaji’ kikosi chake baada ya kutoridhishwa na kiwango cha msimu wa 2025-26.

Kwa namna yoyote ile, ilikuwa ni lazima safu ya ushambuliaji ipitiwe na operesheni hiyo ya kuimarisha kikosi Kwa ajili ya msimu ujao (2026-27).

Hivyo, ameondoka si tu akiwa hajafikia matarajio yake, bali pia hakuweza kutimiza ndoto waliyokuwa nayo mashabiki na hata viongozi wa Yanga wakati wanamng’oa Azam misimu miwili iliyopita.

Related articles

Recent articles