LONDON, Uingereza
WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, ameachia ngazi ikiwa ni miaka isiyotimia miwili tangu alipoingia madarakani kupitia Chama cha Labour.
Hatua hiyo imekuja baada ya shinikizo kubwa la kutaka ajiuzulu, wakosoaji wake wakisema amefeli katika mambo mengi, ikiwamo mzigo mzito wa kodi walionao wananchi, pamoja na mdororo wa huduma za kijamii.
Hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya matokeo ya Uchaguzi mdogo wa Mei, 2026, ambapo Labour ilipoteza makansela takribani 1,500 na halimashahuri 38 nchini nzima.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2029, wanasiasa wengi wa Labour walionesha wasiwasi wao wa Chama hicho kung’olewa madarakani endapo Starmer asingejiuzulu.
Starmer, kwa upande wake, amekiri kusikia baadhi ya wenzake ndani ya Chama wakisema hawana imani na uongozi wake kuelekea Uchaguzi huo.

Taarifa za kujiuzulu kwake zilisikika muda mrefu, ikiwamo kauli ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani, Donald Trump, aliyesema Starmer angebwaga manyanga.
Kwa Uingereza, nafasi ya Waziri Mkuu imekuwa kiti cha moto tangu vuguvugu la nchi hiyo kujitoa Umoja wa Ulaya (Brexit) mwaka 2016.
Baada ya mchakato wa Brexit kupigiwa kura, Waziri Mkuu wa wakati huo, David Cameron, alitangaza kujiweka kando.
Mwaka 2019, ilikuwa ni zamu ya Theresa May, ambaye aliingia madarakani Julai 13, 2026. Alijiuzulu baada ya kukosa uungwaji mkono katika mchakato huo wa Brexit.
Boris Johnson alifuata kwa kuingia madarakani Julai 24, 2019 lakini aliachia ngazi Septemba 6, 2022.
Uamuzi wake wa kujitoa madarakani ulitokana na skendo nyingi, sambamba na wimbi la mawaziri kujiuzulu kwenye uongozi wake.
Liz Truss alishika nafasi yake kuanzia Septemba 6, 2022 lakini alidumu kwenye kiti kwa siku 49 pekee. Akajiuzulu Oktoba 25.
Safari hii, kijiti kilimwangukia Rishi Sunak ambaye alianza majukumu Oktoba 25, 2022 lakini aliachia ngazi Julai 5, 2024.
Kama itakumbukwa, Sunak, ambaye ndiye aliyempisha huyu wa sasa, Starmer, alijiuzulu baada ya Chama cha Labour kupata ushindi kiduchu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2024.


