LONDON, Uingereza
TANGU alipoanguka uwanjani wakati wa fainali za EURO 2020, straika wa timu ya Taifa ya Denmark, Christian Eriksen, amekuwa akivaa kifaa maalumu cha kusaidia mapigo ya moyo (implantable cardioverter defibrillator – ICD).
Eriksen amekuwa na kifaa hicho cha ICD kwenye kifua chake ili kuuhisha mapigo ya moyo endapo yatasimama au kuyarejesha kwenye hali yake ya kawaida endapo litatokea tatizo.
ICD ni kifaa chenye ukubwa wa nusu ya ukubwa wa simu ya mkononi, ambapo nyaya zake huunganishwa moja kwa moja kwenye moyo.

Dk. Amanda Lahti, ambaye pia ni mtafiti wa tiba za michezo, anasema mchezaji au mwanamichezo hupachikwa kifaa hicho baada ya makubaliano.
“Ni makubaliano ya pande zote. Tunapata maoni ya klabu, mchezaji, wakala wake na wataalamu wa afya ili kuona hatari na faida zake,” anasema.
Kwa upande mwingine, siyo Ligi zote kubwa, zikiwamo tano za barani Ulaya, zinaruhusu wachezaji wenye ICD vifuani kuendelea kucheza soka.
Mathalan, Ligi Kuu ya Italia (Serie A) hairuhusu mchezaji mwenye kifaa hicho kucheza. Hivyo, Eriksen aliamua kuondoka Inter Milan na kutua England (Brentford na Manchester United), ambako sheria hazizuii mchezaji kucheza akiwa na ICD.
Hata hivyo, Shirika la Soka la Kimataifa (FIFA) na lile la Ulaya (UEFA) yameruhusu mchezaji mwenye ICD kucheza michuano yake yote (Kombe la Dunia, Ligi ya Mabingwa, n.k.).
Kwa upande wa Ujerumani, pia inaruhusu wachezaji wa aina hiyo kucheza Bundesliga na michuano yote mingine ya ndani. Eriksen alicheza huko msimu uliomalizika (2025-26) akiwa na Wolfsburg.
Dk. Lahti anasema kwa miaka mingi, mchezaji mwenye tatizo la moyo aliambiwa hawezi kuendelea na soka lakini ICD imeleta mabadiliko makubwa.


