TEHRAN, Iran
NI miezi sita sasa tangu Mojtaba Khamenei alipoteuliwa kuwa kiongozi mpya wa Iran baada ya baba yake kuuawa katika shambulizi la kwanza lililofanywa na Marekani na Israel.
Tangu hapo, Mojtaba hajaonekana hadharani wala kusikika, jambo linaloibua wasiwasi juu ya hali yake; amejificha akihofia kuuawa kama baba yake au amefariki?
Viongozi wenzake wa Iran wanadai kuwa Mojtaba yuko hai na amekuwa akitekeleza majukumu yake kama kawaida. Kwa mujibu wao, amejificha kutokana na sababu za kiusalama, huku akiendelea kuuguza majeraha aliyopata katika shambulizi lililomuua mzee wake Februari 28, 2026.
Hata hivyo, kwa wanachi walio wengi, ni ngumu kwa kiongozi, hata kama amejificha, kutoonekana kwa picha, video wala sauti yake kusikika tangu alipoteuliwa wiki ya kwanza ya vita.
Hasa katika kipindi kama hiki, ambacho hali ya usalama si ya kiwango cha kuridhisha, pia uchumi umeyumba kutokana na vita, wengi wanahisi ulikuwa wakati sahihi kusikia chochote kutoka kwa kiongozi.
Iliwashangaza wengi pale Mojtaba aliposhindwa hata kuhudhuria mazishi ya baba yake aliyezikwa kwa heshima kubwa mwezi uliopita (Julai, 2026) nchini Iran.
“Swali lililopo sasa si tu Mojtaba kuwepo au la, bali je, Iran bado inaye kiongozi wake,” anasema Alex Vatanka, mchambuzi wa siasa kutoka Taasi ya Mashariki ya Kati iliyoko Washington, Marekani.
Licha ya wasiwasi huo, bado mamlaka za Iran zimeendelea kusisitiza, kwamba Mojtaba yupo na amekuwa akihudhuria na kuendesha vikao na kutoa maelekezo kwa viongozi wa chini yake katika masuala yote muhimu.
Agosti 10, 2026, Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, alithibitisha hilo aliposema alikutana na Mojtaba na kufanya naye kikao kilichochukua takribani saa saba kumalizika.
Lakini, kwa wananchi bado hawaamini kama kiongozi wao huyo yupo hai. “Tunahitaji kuisikia sauti ya kiongozi wetu au kuona dalili zote za kuthibitisha kuwa yupo kwenye uongozi wa nchi ili kutupa hali ya kujiamini,” anasema mmoja ya wananchi.
Kwa wengine, hasa wasiounga mkono uongozi uliopo, wanasema hakuna ushahidi kuthibitisha kuwa Mojtaba yuko hai. Mmoja wao anasema: “Hakuna ushahidi wa kuwa yuko hai, achilia mbali hayo yanayoelezwa kuwa amekuwa akifanya maamuzi.”


