LOS ANGELES, Marekani
NI miaka 17 imepita tangu staa wa muziki wa Pop, Michael Jackson, alipofariki Juni 25, 2009, lakini sasa ni kama amezaliwa upya tangu filamu ya maisha yake ilipoingia sokoni.
Wiki nne tu baada ya filamu hiyo kuachiwa Aprili 24, 2026, nyimbo zake zimesikilizwa upya mara milioni 40 katika jukwaa la muziki la Spotify, hivyo kufikisha jumla ya wasikilizaji zaidi ya milioni 102.
Wakati huo huo, idadi ya wafuasi wake katika jukwaa la Spotify nao wameongezeka kutoka milioni 29.6 hadi milioni 43.5.
Kama hiyo haitoshi, Michael anashika nafasi ya kwanza kwa upande wa wasanii ‘wanao-trend’ katika jukwaa la Chartmetric.
Kwa upande mwingine, ngoma zake zinazoendelea kuvuna mashabiki wapya, achilia mbali wanaorudia kuzisikiliza, ni ‘Billie Jean’, ‘Beat It’, ‘Human Nature’, ‘Bad’, ‘Don’t Stop ‘Til You Get Enough’, ‘Workin’ Day and Night’, ‘Dangerous’, na ‘Thriller’.
Aidha, licha ya kwamba Marekani ndiyo nyumbani, kwa sasa mashabiki wengi wa Michael kwenye Spotify wanatoka Latin Amerika, ambao wameongezeka kutoka asilimia 33.5 hadi asilimia 35.3.
Katika jukwaa hilo, asilimia 27 wanatoka Hispania, wakati Brazil ina asilimia 14 ya wasilkilizaji wa nyimbo zake duniani.


