Na mwandishi wetu, Gazetini
MAMA mzazi wa aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk. John Pombe Magufuli, Mama Suzana Magufuli, kufariki dunia akiwa nyumbani kwake Chato mkoani Geita baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Kifo cha Mama Suzana, ambaye wengi walimfahamu kama mlezi mkuu na nguzo ya familia ya Hayati Magufuli, kimethibitishwa leo Jumatatu Mei 25, 2026 na mjukuu wake, Jesca Magufuli.
Akizungumzia mziba huo, Jesca amesema bibi yake amefariki dunia majira ya saa 1:00 usiku akiwa nyumbani kwake Chato ambako alikuwa akipatiwa matibabu na uangalizi wa familia.
“Bibi yetu, Mama Suzana Mussa Magufuli, amefariki saa moja usiku nyumbani kwake Chato baada ya kuugua kwa muda mrefu. Taratibu za msiba familia itawajulisha. Bwana ametoa na Bwana ametwaa,” amesema Jesca kwa masikitiko.
Kifo hicho kimeamsha tena kumbukumbu za familia ya Hayati Dk. Magufuli, aliyewahi kuliongoza taifa kuanzia mwaka 2015 hadi 2021, huku Mama Suzana akitajwa kuwa sehemu muhimu ya malezi na mafanikio ya maisha yake ya kisiasa na uongozi.
Katika kipindi chote cha uhai wake, Mama Suzana alibaki kuwa mtu wa karibu wa familia, mwenye msimamo wa unyenyekevu na mlezi aliyethamini maadili ya kazi, nidhamu na utu sifa ambazo mara nyingi zilihusishwa pia na marehemu mwanawe, Dk. Magufuli.


