23.1 C
New York

Tanesco yawahakikishia maafisa huduma kwa wateja mazingira bora ya kazi

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

MKURUGENZI wa Rasilimali Watu na Utawala wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Beatrice Kimoleta, amewahakikishia Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika hilo ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha wanapatiwa nyenzo muhimu zitakazowawezesha kutoa huduma bora na yenye ufanisi kwa wateja.

Kimoleta ametoa kauli hiyo Mei 22, 2026 wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa maafisa hao uliofanyika kwa siku tano jijini Dodoma kuanzia Mei 18, 2026, ukiwa na lengo la kutathmini utendaji kazi na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.

“Kwa uongozi wa Shirika, kipaumbele chetu ni kuhakikisha watumishi wanaohudumia wateja moja kwa moja wanakuwa katika mazingira mazuri ya kazi ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi. Tunawahakikishia kuwapatia nyenzo muhimu ili muendelee kutoa huduma bora kwa wateja,” amesema Kimoleta.

Amesema uongozi wa Shirika unatambua mchango mkubwa wa Maafisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja katika kujenga taswira chanya ya Serikali na Shirika kupitia utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

“Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuwahudumia wateja kwa kujituma. Mchango wenu unajenga taswira chanya ya Serikali na Shirika kwa wananchi. Endeleeni kudumisha uadilifu na weledi katika utendaji kazi wenu,” ameongeza.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutumia mafunzo yaliyotolewa katika mkutano huo kama chachu ya kuongeza ufanisi wa kazi na kuimarisha ushirikiano wa kiutendaji miongoni mwa watumishi hao.

“Kundi hili ni muhimu sana katika kulinda taswira ya Shirika. Ninaamini mafunzo mliyopata yatasaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi katika kazi zenu,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle, ameushukuru uongozi wa Shirika kwa kuwezesha mkutano huo ambao amesema umetoa nafasi kwa maafisa kujadili changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma.

Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, Irene Gowelle,

“Najivunia kuongoza kundi hili kutokana na ufanisi wao mkubwa, hasa wanapokabiliana na changamoto mbalimbali kwa kujitolea kufanya kazi kwa ziada na kuhudumia wateja kwa weledi wa hali ya juu,” amesema Gowelle.

Naye Mwenyekiti wa mkutano huo, Amon Bidebuye, akizungumza kwa niaba ya maafisa wenzake, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na viongozi wa Shirika ili kuendelea kuboresha huduma kwa wateja sambamba na maendeleo ya teknolojia.

Related articles

Recent articles