HONG KONG, China
BINTI wa bilionea Jimmy Lai amesema baba yake anayesota gerezani anakabiliwa na changamoto kubwa ya kiafya, ikiwamo kung’oka meno na kucha.
Lai mwenye umri wa miaka 78, anashikiliwa tangu Desemba, 2020, na sasa huenda akahukumiwa kifungo cha maisha.
Tajiri huyo anashutumiwa kwa makosa ya uhaini, akitajwa kushirikiana na wadau wa nje ya China.
Tangu alipokamatwa miaka takribani mitano iliyopita, familia yake imekuwa ikitilia shaka maisha anayoishi, ikieleza kuwa ananyimwa hata haki ya kupata matibabu.
Hata hivyo, mamlaka za Hong Kong na China zimekanusha mara kadhaa, zikisisitiza kuwa Lai anaendelea vizuri akiwa gerezani.
Katika barua yake kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, familia yake imemuomba ashinikize kuachiwa kwa Lai pindi atakapokutana na Rais wa China, Xi Jinping, hivi karibuni.


