8 C
New York

Mabondia matajiri zaidi duniani

Published:

LOS ANGELES, Marekani

UKIWEKA kando soka, masumbwi ni mchezo mwingine unaofuatiliwa zaidi, ukifuatiwa na mpira wa kikapu. Takwimu zinaonesha hivyo.

Kutokana na ushawishi wake duniani, mchezo wa ngumi umekuwa si tu ajira, bali pia chanzo kikubwa cha utajiri, hasa katika mataifa yaliyoendelea. Katika makala haya, hawa ni mabondia wenye fedha nyingi, kwa mujibu wa Jarida la Forbes. Endelea kusoma.

Floyd Mayweather Jr.

Licha ya kutokupigana pambano lolote la kulipwa tangu mwaka 2017, Mayweather ndiye bondia tajiri zaidi duniani. Dola milioni 400.

Alistaafu akiwa hajawahi kupigwa katika mapambano 50 aliyopanda ulingoni. Atakumbukwa kwa kuwatandika mabondia wakubwa, wakiwamo Pacquiao, Canelo, Conor McGregor, Ricky Hatton na Victor Ortiz.

Saul ‘Canelo’ Alvarez.

Bondia huyo wa kimataifa wa Mexico ana miaka 20 katika ulimwengu wa ndondi za kulipwa. Amepigana mara 68 na kushinda mapambano 63.

Kwa sasa, utajiri wake ni Dola milioni 300, licha ya kwamba alipoteza pambano lililopita alipotandikwa na Terence Crawford.

George Foreman

Hadi anafariki Machi, mwaka huu, ‘Big George’ wa Marekani alishakusanya utajiri wa Dola milioni 300 katika maisha yake ya masumbwi.

Alistaafu akiwa na rekodi ya kushinda mapambano 76. Ana historia ya kuwa bingwa wa dunia mwenye umri mkubwa zaidi (miaka 45).

Manny Pacquiao

Rekodi yake ya kushinda mara 62 katika mapambano 71 inamfanya Pacquiao kuwa mmoja ya mabondia wenye heshima kubwa duniani.

Si tu heshima, pia raia huyo wa Ufilipino amevuna fedha nyingi kupitia ndondi. Pacquiao ana utajiri wa Dola milioni 220.

Jake Paul

Licha ya kwamba ana mapambano sita pekee tangu alipoingia kwenye ulimwengu wa ngumi za kulipwa, ameshatengeneza utajiri wa Dola milioni 200.

Paul (28), alivuna Dola milioni 40 katika pambano lake la Novemba, mwaka jana, dhidi ya mkongwe Mike Tyson. Pia, akachota Dola milioni 92 alipopigwa na Anthony Joshua katika pambano lililopita.

Oscar De La Hoya

Bondia huyo raia wa Marekani alistaafu ndondi akiwa na rekodi ya kushinda mara 39 na kupigwa mara sita pekee katika mapambano yake.

Utajiri wake kwa sasa ni Dola milioni 200, akiwahi kuzipiga na mastaa wakubwa, wakiwamo Manny Pacquiao na Floyd Mayweather. Kwa sasa, De La Hoya ni promota wa ngumi.

Anthony Joshua

Wakati fulani, ‘AJ’ aliwahi kuwa bingwa wa dunia mara mbili. Pia, alikuwa bingwa wa michuano ya Olimpiki ya mwaka 2012.

Utajiri wake ni Dola milioni 199 na sehemu ya fedha hizo alivuna kupitia mapambano yake mawili dhidi ya Oleksandr Usyk, Andy Ruiz Jr na Francis Ngannou.

Tyson Fury

Mashabiki wake nchini Uingereza wanamfahamu kwa jina la ‘Gypsy King’. Usyk hajawa kwenye kiwango bora hivi karibuni, ambapo amepigwa mara zote mbili alizokutana na Oleksandr Usyk.
Hata hivyo, bado Fury mzaliwa wa jijini Manchester ana utajiri wa Dola milioni 160. Pambano lake l mwisho dhidi ya Usyk lilimpa Dola milioni 81.

Lennox Lewis

Muingereza huyo alikuwa bondia wa viwango vya juu katika miaka ya 1990, ikikumbukwa kuwa alitwaa medali ya dhahabu wakati wa michuano ya Olimpiki ya mwaka 1988.
Lewis ameshastaafu. Aliondoka kwenye masumbwi akiwa ni bingwa mara tatu wa Dunia. Utajiri wake ni Dola milioni 140.

Oleksandr Usyk

Ana utajiri wa Dola za Marekani milioni 120. Ushindi wake katika mapambano yake mawili dhidi ya Tyson Fury mwaka jana unatajwa kumpa fedha nyingi zaidi katika maisha yake ya ndondi.
Usyk, raia wa Ukraine mwenye umri wa miaka 38, alivuna kiasi kikubwa cha fedha alipopigana na Anthony Joshua ‘AJ’ na Daniel Dubois aliyempiga kwa ‘KO’ katika pambano lake la hivi karibuni.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img