10.6 C
New York

Magenge ya uhalifu yanavyoitesa Serikali ya Mexico – [3]

Published:

SINALOA, Mexico

UNAPOITAJA historia ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini Mexico, hutaacha kuyagusa magenge makubwa matano. Makala haya yanachambua kwa kina zaidi. Endelea nayo …

Tuanze na Sinaloa Cartel. Kundi hilo lilianza kugombea mamlaka ya mtandao wa uhalifu baada ya kuona Gulf Cartel limepoteza mwelekeo alipokamatwa kiongozi wao, Osiel Cardenas mwaka 2003.

Mwaka 2006, Sinaloa Cartel chini ya kiongozi wake, Joaquin Guzman ‘El Chapo’, liliunda shirikisho kwa kushirikiana na magenge mengine ya mjini Sinaloa.

Baadaye, El Chapo akawa kiongozi wa uhalifu anayesakwa zaidi nchini Mexico, pia akitajwa kuwa na utajiri wa Dola bilioni moja.

Chini yake, Sinaloa Cartel liliweza kulizima kundi la Juarez Cartel baada ya mapigano makali yaliyogharimu maisha ya watu zaidi ya 12,000 ya kuwania kudhibiti mtandao wa dawa za kulevya nchini Mexico.

Inaelezwa kuwa ushindi huo ulikuja baada ya Sinaloa Cartel kushirikiana na vikundi vingine, ikiwamo Los Mexicles, Artistas Asesinos na Gente Nueva, kuwashambulia Juarez Cartel.

Pia, zipo stori kwamba hata Juarez Cartel hawakupigana peke yao, bali nao walipewa sapoti na magenge mengine yaliyokuwa tishio wakati huo ya La Linea na Barrio Azteca.

El Chapo alikamatwa na kisha kutoroka mwaka 2015, kabla ya kudakwa tena mwaka 2016 na kukabidhiwa mikononi mwa vyombo vya dola vya Marekani mwaka 2017.

Baadaye, El Chapo alifichua kuwa alikuwa akiwapa rushwa waliokuwa marais wa Mexico, Enrique Pena Nieto na Felipe Calderon, madai ambayo hata hivyo wote walisema hayakuwa na ukweli.

Mwaka 2019, alihukumiwa kifung cha maisha gerezani na kumwachia Ismael Zambada ‘El Mayo’ kuwa kiongozi wa Sinaloa Cartel.

Hata hivyo, Zambada naye hakudumu kwani alidakwa na vyombo vya dola mwaka 2024 na kisha kukabidhiwa mikononi mwa Shirika la Ujasusi la Marekani mwaka 2025.

Mwaka 2023, kukamatwa kwa mtoto wa El Chapo, Ovidio Guzman, kulizua mapigano makali kati ya kundi hilo na polisi mjini Sinaloa. Polisi walilazimika kutumia mashambulizi ya anga kuhimili vishindo vya kundi hilo.

Februari, 2026, Serikali ya Marekani ilitangaza kuwa ingempa kitita cha Dola milioni 10 mtu yeyote ambaye angetoa taarifa za kufanikisha kukamatwa kwa kiongozi wa sasa wa Sinaloa Cartel.

Itaendelea …

Related articles

Recent articles