Na Ramadhan Hassan, Gazetini – Dodoma
TANZANIA inatarajiwa kuwa kitovu cha mijadala ya kimataifa kuhusu ukuzaji viumbe maji baada ya kuteuliwa kuwa mwenyeji wa Kongamano la Dunia la Ukuzaji Viumbe Maji na Kongamano la Afrika, yatakayofanyika jijini Dar es Salaam, kuanzia Desemba 1 hadi 4, mwaka huu.
Kongamano hilo linatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji, kukuza ushirikiano wa kimataifa na kuimarisha maendeleo ya sekta ya ukuzaji viumbe maji nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, leo Novemba 24, 2026, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Bashiru Ally, amesema Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaandaa mikutano hiyo ya kimataifa.
Amesema Tanzania imepewa jukumu la kuwa mwenyeji na mwenyekiti wa Kongamano la Dunia la Ukuzaji Viumbe Maji pamoja na Kongamano la Afrika kwa mwaka 2026, akieleza kuwa hatua hiyo ni heshima kubwa kwa nchi katika tasnia hiyo.
Amesema mikutano hiyo itafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, huku Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi na kuzindua kongamano hilo Desemba 2, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Dkt. Bashir, kongamano hilo linatarajiwa kushirikisha washiriki zaidi ya 1,000 kutoka nchi 100 duniani, wakiwemo wataalamu, wadau na wawekezaji katika sekta ya ukuzaji viumbe maji.
Amesema katika siku hizo nne, kutakuwa na maonesho, warsha, vikao vya wanafunzi na majadiliano yatakayowezesha washiriki kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili maendeleo ya sekta hiyo duniani.
Dkt. Bashir amesema kuwa fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mikutano hiyo itasaidia kuitangaza nchi kimataifa, kuvutia wawekezaji na kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya ukuzaji viumbe maji.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuendeleza sekta hiyo, ikiwemo kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa mikopo kwa wananchi na wawekezaji wanaotaka kujihusisha na shughuli za ukuzaji viumbe maji.


