Na mwandishi wetu, Gazetini – DAR
SIKU ya Wanaume Duniani husherehekewa Novemba 19 ya kila mwaka, kama ilivyofanyika Alhamisi ya wiki hii, licha ya kwamba bado haijatambulika rasmi kwenye kalenda ya Umoja wa Mataifa [UN], tofauti na ile ya Wanawake ya Machi 8 [kila mwaka].
Historia inakumbusha, kwamba Siku ya Wanaume ilianzia kupigiwa chapuo kutambulika na kusherehekewa kimataifa katika miaka ya 1960.
Mwaka 1968, mwandishi wa habari wa Marekani, John P. Harris, aliandika makala yake katika jarida la Salina, akieleza kuwa wanawake kutengewa Machi 8 kama Siku yao duniani ni kupuuza mchango wa wanaume kwenye jamii zao.
Harris alieleza pia, wanaume wamekuwa wakivuja jasho jingi kupambania familia, jamii na mataifa yao lakini hakuna Siku yao maalumu ya kuenzi na kutambua kile wanachokifanya.
Wazo lake hilo lilipata uungwaji mkono katika vyombo vya habari vingi hapo baadaye na hatimaye Malta ikawa nchi ya kwanza kuandaa kongamano la Siku ya Wanaume mwaka 1994. Sherehe za aina hiyo zilionekana pia Marekani na Australia, ambazo zote ziliamua kuichagua Februari.
Miaka mitano baadaye, Trinidad and Tobago nayo ikaitambua rasmi Siku ya Wanaume duniani, ambapo muasisi wake alikuwa Jerome Teelucksingh, ambaye alitaka iwe Novemba 19 ya kila mwaka kwa kuwa ndiyo ‘birthday’ ya baba yake.
Novemba 19, 2009, Ghana na Afrika Kusini zilikuwa nchi za mwanzoni kabisa kushuhudiwa kuwa na mikusanyiko ya kutambua na kusherehekea Siku ya Wanaume.
Baadaye, nchi zingine zilifuata, zikiwamo Botswana, Tanzania na Zimbabwe [2011], Burundi [2012] na Visiwa vya Shelisheli [2012], kisha Nigeria [2022].
Nje ya Afrika, mataifa mengine yenye Siku ya Wanaume, licha ya kwamba siku inaweza kutofuatiana ni Canada, Colombia, Cuba, Grenada, Jamaica, China, India, Pakistan na Singapore.
Pia, miongoni mwazo zipo pia Bosnia, Denmark, Ufaransa, Hungary, Ireland, Romania, Ukraine, Uingereza, Scotland, na New Zealand.
Makala fupi haya yameandaliwa kwa msaada wa vyanzo vya habari vya kimataifa.


