LAGOS, Nigeria
HALI ya taharuki imezuka baada ya taarifa ya boti iliyokuwa na abiria zaidi ya 300 kuzama nchini Nigeria, tovuti ya Daily Post imeeleza.
Boti hiyo ilikuwa ikisafiri kutoka Ayama kwenda Ukubie katika Jimbo la Bayelsa, huku wengi kati ya abiria wakiwa hawajulikani walipo.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, abiria hao walikuwa wakielekea msibani katika eneo la Ukubie. Ajali hiyo ilitokea Ijumaa ya wiki hii, muda mfupi tu baada ya boti hiyo kupita eneo la Oweikorogha.
Aidha, aliyethibitisha kutokea kwa tukio hilo ni Msemaji wa Polisi wa Jimbo la Bayelsa, Musa Muhammad, akidai kuwa timu yake ilifika na kuanza operesheni ya uokoaji.
Hata hivyo, kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Majini nchini Nigeria katika Jimbo la Bayelsa, Comrade Ogoniba Ipigansi, amesema timu ya uokoaji inaendelea na zoezi la kutafuta miili na taarifa za abiria hao.


