BEIJING, China
PICHA za video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonesha Rais wa Marekani, Donald Trump, akiwa amefumba macho wakati vikao vya mkutano wa kilele wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Asia na Pasifiki (APEC) vikiendelea nchini China, zimeibua mijadala mzito, wengine wakihusisha na utimamu mdogo wa afya yake.
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa, tukio hilo lilitokea wakati viongozi wengine wakiendelea kutoa hotuba zao katika ukumbi wa mkutano huo unaojadili masuala ya biashara na uwekezaji.
Mbali na wenye hoja ya afya na umri wake, baadhi ya wakosoaji wamedai kuwa huenda Rais Trump aliamua kuchapa usingizi kwa kupuuzia au kutokuona uzito wa hotuba za viongozi wenzake.
Hata hivyo, wapo waliogoma kukubaliana na tafsiri hizo, wakieleza kuwa kuonekana kwa kiongozi akiwa amefumba macho hakuthibitishi moja kwa moja kuwa alikuwa amelala, na badala yake huenda alikuwa akisikiliza kwa umakini tafsiri ya hotuba kupitia vifaa vya masikioni.
Pia, hoja hiyo inajengwa na msingi, kwamba huenda kiongozi huyo alikuwa akikabiliwa na uchovu wa kawaida unaotokana na safari ndefu za ndege na mabadiliko ya saa (jet lag) kati ya Marekani na Bara la Asia.
Lakini, hadi sasa, ofisi ya Rais wa Marekani (Ikulu ya White House) haijatoa taarifa rasmi kuzungumzia picha hizo zinazosambaa mitandaoni.
Mkutano huo wa kilele wa APEC unakutanisha wakuu wa nchi na serikali 21 zinazopakana na Bahari ya Pasifiki kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na biashara huria.


