16.9 C
New York

Njaa yatesa wakimbizi 14,000 wa Ethiopia

Published:

NAIROBI, Kenya

SHIRIKA la Msalaba Mwekundu nchini Kenya limesema zaidi ya wakimbizi 14,000 waliokimbia mapigano nchini Ethiopia wanakabiliwa na uhaba wa chakula, maji safi na vyoo katika eneo la Moyale, kaunti ya Marsabit nchni Kenya.

Kati yao, zaidi ya 10,900 wamehifadhiwa katika kambi sita, huku wengine zaidi ya 4,000 wakiishi na jamaa na marafiki katika jamii zinazowapokea.

Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo la Upper Eastern, Malik Adan, amesema wakimbizi hao wanahitaji msaada wa dharura wa chakula, maji safi, vifaa vya usafi na vyoo ili kukidhi mahitaji yao na kupunguza hatari ya milipuko ya magonjwa, ikiwamo kuhara.

Amesema shirika hilo tayari limewapatia baadhi ya wakimbizi mahema, blanketi, mikeka, vyombo vya jikoni, huduma ya kwanza pamoja na chakula maalumu kwa watoto wadogo na akina mama.

Hata hivyo, Serikali ya Kaunti ya Marsabit, ambayo imeahidi kutoa mchele na maharagwe, inakabiliwa na changamoto ya kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakimbizi hao.

Mohamed Nane, msimamizi wa kambi ya Manyatta Madrassa, amesema baadhi ya familia zinazowahifadhi wakimbizi zinaishi na zaidi ya watu 20 wa ziada, hali inayoongeza shinikizo kwa rasilimali chache walizonazo.

Nane amezitaka serikali na mashirika ya kibinadamu kuingilia kati haraka ili kutoa msaada unaohitajika kwa wakimbizi na familia zinazowapokea.

Kwa upande wake, Bashir Tufa, mmoja wa wakimbizi hao, amesema alilazimika kukimbia Ethiopia kutokana na mapigano makali kati ya vikosi vya maeneo ya nne na tano.

Tufa amesema mapigano bado yanaendelea, huku wakimbizi wakiwa katika hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu usalama wao na muda watakaolazimika kukaa nchini Kenya.

Hali hiyo imeongeza uhitaji wa msaada wa kibinadamu katika eneo la Moyale, huku wakimbizi wakihitaji huduma muhimu za kuwawezesha kuishi katika mazingira salama na yenye kuzingatia afya na usafi.

Related articles

Recent articles