LONDON, Uingereza
TEKNOLOJIA ya kumsaidia mwamuzi kwa kutumia marejeo ya video [VAR] ilitambulishwa Ligi Kuu ya England [EPL] kwa lengo la kuondosha utata wa makosa ya wazi.
Hata hivyo, mara kadhaa imetokea kwa VAR kuzua mijadala juu ya ufanisi wake, ambapo katika baadhi ya mechi imekuwa ikisababisha maumivu kwa timu moja au nyingine.
Mathalan, katika mchezo wa ‘dabi’ kati ya Manchester United na Manchester City, Bodi ya Waamuzi ya EPL [PGMOL] ilikiri kuwa VAR ilifanya kosa kuliruhusu bao la Erling Haaland.
Hata hivyo, hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa teknolojia hiyo kuwapotosha waamuzi wa kati tangu ilipoanza kutumika kwenye Ligi Kuu hiyo ya EPL.
Ishu ya Haaland na United [2026]
Katika mchezo dhidi ya Man United, straika Haaland ndiye aliyefunga bao pekee. Mwamuzi wa kati alilikataa kwa madai kuwa mfungaji alikuwa ameotea kabla ya kufunga. VAR ilitengua uamuzi huo na kuruhusu bao.
Hata hivyo, PGMOL iliibuka baadaye na kusema VAR ilipotosha na hilikuwa bao halali lililoipa ushindi Man City iliyokuwa pungufu baada ya Phil Folden kupewa kadi nyekundu.
Kilichoikuta Palace [2023]
VAR ilifanya kituko kingine katika mechi kati ya Brighton na Crystal Palace, ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1. Kama si teknolojia hiyo, Brighton wangepata ushindi wa mabao 2-1.
Brighton ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Pervis Estupinan lakini VAR ililikataa kwa madai kuwa alikuwa ametoea. Uamuzi huo ulikuja kukosolewa na PGMOL, ambapo Bodi hiyo ililazimika kuiomba radhi Brighton.
Toney na Arsenal [2023]
Arsenal wakiwa wanaongoza kwa bao 1-0 hadi dakika ya 74, makosa ya VAR yalisababisha wakose pointi tatu mbele ya Brighton. Teknolojia hiyo haikuona kama Christian Norgaard alikuwa kwenye eneo la kuotea wakati anatoa asisti kwa Ivan Toney aliyeifungia Brigton bao la kusawazisha.
Ni baada ya mechi hiyo, Mkuu wa Bodi ya Waamuzi, PGMOL, Howard Webb, aliiomba radhi Arsenal akikiri VAR haukuwa sahihi kuliruhusu bao hilo la Toney.
Diaz na Tottenham [2023]
Ni katika mchezo uliochezwa Anfield na Liverpool kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tottenham. VAR ilikataa kimakosa bao halali la Luis Diaz wa Liverpool.
Diaz aliifungia Liverpool bao la kipindi cha kwanza lakini VAR ilishindwa kugundua kuwa ‘off-side’ yake iliuliwa na beki wa Tottenham, Cristian Romero. PGMOL ilikuja kukiri kosa hilo na kuomba radhi.
Cornet na Chelsea [2022]
West Ham United wakiwa nyuma kwa mabao 2-1, staa wake, Maxwel Cornet aliisawazishia akitumia uzembe wa kipa wa Chelsea, Edouard Mendy. Mwamuzi wa kati, Andrew Madley, aliruhusu bao hilo.
Lakini, VAR ilimwita kwa madai kuwa Mendy alishachezewa rafu wakati wa shambulizi hilo. Hivyo, mwamuzi Madley aliamua kulikataa bao hilo la West Ham. Baadaye, PGMOL ilikiri kuwa uamuzi wa VAR haukuwa sahihi.


