26.3 C
New York

Umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma sasa asilimia 99

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SASA wananchi wa Dodoma watapata umeme unaozalishwa katika Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) kupitia njia ya usafirishaji wa nishati hiyo kutoka Chalinze mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba, njia hiyo ya kusafirisha Umeme ya Msongo wa Kilovolti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma imeshakamilika kwa asilimia 99.

Mhandisi Mramba aliyasema hayo Agosti 18, 2026, wakati akikagua hatua za mwisho za utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Njia ya Kusafirisha Umeme ya Chalinze–Dodoma yenye urefu wa kilomita 345.

Ifahamike kuwa Mradi huo ni pamoja na upanuzi wa Vituo vya Kupoza na Kusambaza Umeme vya Chalinze mkoani Pwani na Zuzu jijini Dodoma.

Amesema ujenzi wa njia hiyo umefikia asilimia 99, huku upanuzi wa Kituo cha Zuzu ukiwa umefikia asilimia 98 na kwamba wataalamu wamekamilisha maandalizi ya kuanza kuwasha umeme katika njia hiyo.

“Kituo cha Zuzu kipo tayari katika hatua za mwisho kabisa. Wataalamu wamenieleza waatanza kuwasha kwa majaribio katika kituo. Umeme utaanza kufika Dodoma kutoka Bwawa la Julius Nyerere kupitia Chalinze hadi kufika Dodoma,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mwandisi Mramba aliongeza kuwa kukamilika kwa njia hiyo ya kV 400 ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa usafirishaji wa umeme nchini.

Alisema: “Ni kwa kuwa itapokea umeme unaozalishwa katika Bwawa la Julius Nyerere na kuusafirisha kutoka Chalinze hadi Dodoma, ambako utaingizwa kwenye Gridi ya Taifa na kusambazwa kwenda maeneo mbalimbali nchini.”

Wakati huo huo, alisema wanufaika wakubwa wa mradi huo ni Reli ya SGR, akifafanua kuwa njia ya umeme inayotumika kwa ajili ya SGR ilikuwa ikitumika pia kwa matumizi ya watumiaji wengine.

“Hivyo basi, kukamilika kwa njia hiyo kutawezesha watumiaji wengine kuondolewa kwenye njia inayotumiwa na SGR, hivyo reli hiyo kuwa na njia yake ya umeme kwa matumizi yake,” alisema.

Aidha, aliongeza kuwa kukamilika kwa njia hiyo ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma kutatua changamoto ya kuzimika kwa Gridi ya Taifa, kama ilivyotokea hivi karibuni.

“Mradi huo ni miongoni mwa miradi muhimu kwa nchi, ambapo unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 kwa takribani Shilingi bilioni 600, ukiwa ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kusafirisha umeme inayotekelezwa nchini.

Mbali na Dodoma, Mwandisi Mramba alitaja maeneo mengine yatakayonufaika na njia hiyo kuwa ni mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Tabora na Kigoma, pamoja na Singida kwa upande wa Magharibi, na kwa kaskazini ni Manyara, Arusha na Kilimanjaro.

Related articles

Recent articles