Na mwandishi wetu, Gazetini
USAMBAZAJi wa umeme unaotekelezwa na Wakala wa Nishati nchini (REA) umeendelea kubadilisha maisha ya wananchi, wakiwamo wa vitongojini.
Mpango uliopo ni kuhakikisha nishati ya umeme inawafikia wananchi katika vitongoji vyote 64,359 ifikapo mwaka 2030.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, kwa sasa tayari asilimia 62.4 ya vitongoji vimefikiwa na huduma ya umeme.
Mhe. Balozi Kingu aliyesema hayo wiki chache zilizopita wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Mwamlula katika Kijiji cha Mseko na Kitongoji cha Kipeke katika Kijiji cha Masagi Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
Hayo yamesemwa Julai 15, 2026 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu, wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Mwamlula katika Kijiji cha Mseko na Kitongoji cha Kipeke katika Kijiji cha Masagi Wilaya ya Iramba Mkoani Singida.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Thomas Mbaga, alisema Mkoa wa Singida una jumla ya vitongoji 2,289, kati ya hivyo vitongoji 1,196, sawa na asilimia 52.25, tayari vimeunganishiwa umeme.
Aliongeza kuwa vitongoji 1,093, sawa na asilimia 47.75, bado havijafikiwa na huduma hiyo na kwamba utekelezaji wa miradi unaendelea kupitia miradi ya HEP IIA itakayofikisha umeme katika vitongoji 127 na HEP IIB vitongoji 377.


