26.5 C
New York

Jaji Lila: Tume yetu imepewa jukumu la kubaini wahusika wa ghasia

Published:

MWENYEKITI wa Tume ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Shaban Ally Lila, amesema Tume hiyo ina jukumu tofauti na Tume ya Rais iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Mstaafu Othman Chande.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam leo, Jumatat, Agosti 24, 2026, Jaji Lila amesema Tume ya awali ilijikita katika kuchunguza matukio ya ghasia yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ikiwemo kubaini aina ya vurugu, ghasia na uvunjifu wa amani uliojitokeza.

Amesema tofauti na Tume hiyo, Tume anayoiongoza imepewa jukumu la kwenda hatua zaidi kwa kuchunguza na kubaini watu waliohusika katika kupanga, kufadhili, kuratibu na kutekeleza matukio hayo ya ghasia.

“Sisi tumepewa jukumu la kwenda kuangalia wahusika ni kina nani, waliopanga, walioratibu, waliofadhili, waliotekeleza. Halafu pia tuangalie masuala ya madhara kwa maana ya watu wameumia, watu wamefariki kutokana na ghasia zile, nani wahusika, na aina na kiasi cha nguvu kilichotumika kwenye kudhibiti zile ghasia,” amesema Jaji Lila.

Amesema Tume pia itachunguza aina na kiwango cha nguvu kilichotumika katika kudhibiti ghasia hizo, ili kubaini iwapo hatua zilizochukuliwa zilizingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Akizungumzia madhara yaliyotokana na ghasia hizo, Jaji Lila amesisitiza umuhimu wa kuchunguza kwa kina wahusika na matukio yaliyosababisha watu kujeruhiwa au kupoteza maisha.

“Thamani ya mtu hailinganishwi na kitu kingine chochote,” amesema.

Tume hiyo, maarufu kama Tume ya Jaji Lila, iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa rasmi Agosti 7, 2026, ikiwa na jukumu la kuchunguza wahusika wa ghasia na ukiukwaji wa sheria katika matukio yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Tume hiyo inaongozwa na Jaji Lila na inahusisha pia majaji wastaafu pamoja na majaji kutoka nje ya Tanzania.

Related articles

Recent articles