WASHINGTON DC, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump, amezitaka kujiandaa na kibano nchi zitakazoipa ushirikiano Iran. Kauli hiyo ni mwendelezo wa uhusiano mbaya uliopo kati ya mataifa mawili hayo.
Katika taarifa yake kupitia mtandao wa kijamii wa Truth Social, Rais Trump amesema Iran imeshindwa kutumia ‘fursa’ ya kumaliza vita, hivyo ijiande na anguko kubwa la kiuchumi.
Rais Trump alienda mbali zaidi na kusema nchi yoyote itayofanya biashara na Iran nayo itaingia kwenye dhahama ya kukwamishwa kiuchumi.
“Nchi yoyote itakayoruhusu taasisi zake za kifedha, biashara, viwanja vya ndege, au mashirika ya serikali kuisaidia Iran, itakumbana na shida hiyo hiyo,” amesema Rais Trump.
Hata hivyo, wafuatiliaji wa siasa za kimataifa watakumbuka kuwa hii si mara ya kwanza kwa Rais Trump kutishia kuweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran.
Tayari Marekani imeweka vikwazo dhidi ya mafuta ya Iran, sekta za meli na fedha, lengo likiwa ni kudhohofisha uchumi wa Taifa hilo la Kiarabu.
Katika hilo la mafuta, Marekani imekuwa ikizuiwa nishati hiyo kuingia na kutoka Iran, pia ikizipa tishio kampuni zinazojaribu kufanya biashara na nchi hiyo.


