Na mwandishi wetu, Gazetini
ALIZALIWA Agosti 7, 1876 mjini Leeuwarden, Uholanzi. Akitokea katika familia tajiri, Mata Hari akiwa mdogo aliweza kupata kila alichokitaka kutoka kwa wazazi wake.
Hata hivyo, mambo yalibadilika ghafla akiwa na umri wa miaka 13. Baba alifilisika na hatimaye aliikimbia familia. Miaka miwili baadaye, Mata alimpoteza mama, hivyo akaanza kuishi kwa ndugu.
Akiwa binti wa umri wa kuolewa, alibahatika kukutana na tangazo gazetini. Tangazo la mwanaume aitwaye John Rudolf MacLeod, ambaye alikuwa anatafuta mchumba.
Baada ya kuwasiliana, hatimaye walianzisha safari yao ya mapenzi, wakati huo MacLeod akiwa amemzidi Mata kwa miaka 20.
Ndoa ilifuata na hatimaye walipata mtoto wa kiume, ambaye hata hivyo aliuawa kwa kupewa sumu akiwa na umri wa miaka miwili tu.
Hata hivyo, waliachana mwaka 1897 na MacLeod kuondoka na binti yao na kumtelekeza Mata pasi na malipo yoyote ya kumuwezesha kuishi.
Mata alihamia Paris, Ufaransa, na huko akaanza kujiingiza katika sanaa ya uanamitindo ili kujipatia kipato. Miaka michache baadaye, akawa maarufu barani Ulaya, hasa katika miji mikubwa ya Vienna na Monte Carlo.
Wakati huo, Mata akawa anaishi katika hoteli za kifahari (nyota tano) na tayari akawa amejiingiza katika unenguaji (kucheza muziki majukwaani), kazi iliyomuongezea umaarufu na kupato.
Hapo ndipo Mata akawa anapata mialiko ya kwenda kutumbuiza katika hafla za familia za kitajiri, ikiwamo ya aliyekuwa kiongozi wa Ujerumani, Wilhelm II.
Kupitia kazi hiyo, akaweza kujisogeza na kuwa na ukaribu na wanasiasa, wanadiplomasia na viongozi wa kijeshi waliokuwa wakimlipa vizuri kutokana na burudani yake.
Kadiri siku zilizosogea, umaarufu wake ulianza kushuka, hiyo ikitokana na vijana wengi kuanza kuiga unenguaji wake, hivyo kuchukua baadhi ya dili zilizokuwa zikimpa fedha nyingi jijini Paris.
Vita ya Kwanza ya Dunia ilipoanza mwaka 1914, mambo yakawa mabaya zaidi kwa Mata. Hali ya kiuchumi ikawa mbaya na hata kushindwa kumudu kuishi kwenye hoteli za kifahari.
Akiwa amezingirwa pia na madeni, ndipo ilipokuja ofa ya Serikali ya Ujerumani, ikimtaka aisaidie kunasa taarifa za baadhi ya wapinzani wake wakati wa Vita hivyo.
Ujerumani ilimuahidi kumlipia madeni yote, pamoja na kumuongeza kiasi kizuri cha fedha endapo angekubali. Mata akaanza kazi.
Akiwa kwenye majukumu, Mata akapokea ofa nyingine. Safari hii, Ufaransa ilimuahidi kumlipa mara mbili ya fedha alizokuwa akilipwa na Wajerumani. Akakubali.
Ulikuwa ni mtego. Ufaransa haikuwa na shida na huduma yake, bali ilitaka iwe naye karibu ili imchunguze na kubaini kama ni kweli anaisaidia Ujerumani katika shughuli za ukachero.
Wakat huo huo, Uingereza nayo ilishamtilia shaka, kwamba ni kachero wa Ujerumani, hivyo nayo kupitia Shirika lake la Ujasusi ikawa inafuatilia kila hatua ya nyendo zake.
Februari 13, 1917, Mata alikamatwa jijini Paris, na kufunguliwa mashitaka ya uhaini. Miezi michache baadaye (Oktoba 15, 1917), akiwa na umri wa miaka 41, alinyongwa.


