WASHINGTON DC, Marekani
MAREKANI imetangaza kuwa itafikia makubaliano na Iran ndani ya siku mbili zijazo juu ya kufungua Mlango-Bahari wa Hormuz na kurejesha utulivu Mashariki ya Kati.
Aliyesema hayo ni Katibu Mkuu wa Hazina ya Marekani, Scott Bessent, akisema mazungumzo yao na viongozi wa Iran yanaendelea vizuri, akiamini mwafaka utafikiwa hivi karibuni.
“Tuko kwenye mazungumzo na Iran na nafikiri kuna uwezekano wa leo (Agosti 4, 2026, au kesho kufungua Mlango-Bahari wa Hormuz …” amesema.
Hormuz ni njia muhimu ya maji, ikitajwa kutumika kupitisha asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia zinazoingia kwenye soko la dunia.
Kwa muda sasa, Iran imekuwa ikiifunga na kusababisha adha kubwa ya uhaba wa mafuta, hivyo kupanda kwa bei ya nishati muhimu hiyo.
Alipoulizwa kama Iran itaendelea kutoza malipo kwa meli zitakazopita Hormuz, Bessent alisema hapana, akisisitiza kuwa Mlango-Bahari huo utakuwa huru kwa yeyote kutumia.


