27.2 C
New York

Hao ni wachambuzi au ‘wachafuzi’ wa Bongo Fleva?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

KICHEFUCHEFU! Ndicho unachoweza kuhisi pindi tu unapoingia kwenye mitandao ya kijamii na kukutana na hao wanaojiita ‘wachambuzi’ wa muziki wa kizazi kipya (Bongo Fleva). Wachambuzi au wachafuzi?

Kwa msingi wa jina, ungetarajia kuona wakichambua muziki, sivyo? Bila shaka. Walitakiwa kujikita katika kuchambua muziki. Kutoa elimu juu ya aina ya muziki, ‘beat’, tungo au mahadhi ya wimbo wa msanii fulani.

Kwa ufupi, kwa jina la wachambuzi, ulitarajia kuona wakiwa ni watu wenye uelewa mkubwa wa muziki. Labda ni wasanii, maprodyuza au wakufunzi wa vyuo vya sanaa hiyo. Watu wanaoujua muziki.

Nitakupa mfano mdogo. Katika soka, pia tunao wachambuzi. Si wote walicheza lakini wana uelewa mkubwa wa kazi yao, wengine wakijiongeza kwa kusomea taaluma ya ukocha.

Unapomsikiliza mtu wa aina hiyo kupitia redio, kumtazama kupitia televisheni/mitandao au kumsoma gazetini, unaliona soka tu na siyo kunanga maisha binafsi ya mchezaji, kocha, au kiongozi wa klabu husika.

Je, Bongo Fleva inao wachambuzi wa aina hiyo, ambao wana ujuzi wa kuzungumzia udhaifu au ubora wa wimbo kiufundi?

Ukija kwa hao wanaojiita wachambuzi kwa upande wa Bongo Fleva, ni ngumu kupata neno linalofaa kuliko kuita wanachokifanya kuwa ni kichefuchefu.

Kama si njaa, basi ni kiu ya kujulikana au kuongeza umaarufu kiduchu walionao. Nini kingine cha maana? Hakuna.

Wengi wao wamejiingiza na kujitafutia eneo la kuishi kwenye maisha ya mastaa. Wamejikita kuzungumzia maisha binafsi ya wanamuziki na si kuchambua ubora na udhaifu wa kiufundi wa nyimbo.

Kamba msanii fulani ana nyumba, mwingine ameachana na mkewe, au yule anatoka na fulani. Uchambuzi au uchafuzi wa Bongo Fleva? Takataka!

Hata wanapojaribu mara chache kuzungumzia nyimbo zenyewe, hawaoneshi kuwa wana weledi katika kuifanya kazi hiyo, zaidi ya kusifia au kuponda.

Ukimuuliza wimbo huo una uzuri au ubaya gani, hana anachoweza kukwambia kiufundi juu ya aina ya mdundo (beat), tungo, mahadhi, n.k.

Kama atauponda wimbo, basi ni kwa sababu yeye si mfuasi wa kambi ya msanii huyo. Kama ataisifia, basi ujue kula, kulala na kuvaa kwake kunamtegemea msanii huyo.

Ni kweli uchambuzi wa muziki ni fursa nyingine mpya kwenye Bongo Fleva, lakini si kila mtu anapaswa kuikurupukia na kuifanya.

Si mbaya walioamua kuwa ‘chawa’ wakabaki huko ili kutokuichafua tasnia ya uchambuzi, ambayo kimsingi haihitaji yeyote mwenye wafuasi mitandaoni, bali wenye weledi wa muziki.

Related articles

Recent articles