Na Hassan Mwasha, Gazetini
KUONDOKA Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) haikutosha kwa Mchungaji Peter Msigwa. Akahamia kwa washindani wao wakubwa katika siasa za Tanzania, CCM.
Kama hiyo haitoshi, Mchungaji Msigwa akajipa kazi ya kuishughulikia CHADEMA. Akavaa mabomu ya kuichafua Chama hicho kila alipopata nafasi. Kwa ufupi, akawa mpinzani wa mkubwa wa CHADEMA kuliko hata CCM yenyewe!
Aliifanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa wakati wa mikutano ya kampeni za Urais kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Video za kauli zake za ‘shombo’ zipo na zitaendelea kuishi mitandaoni. Ndiyo uzuri wa teknolojia.
Katika moja ya kauli zake maarufu wakati huo, kana kwamba alishapanga kuzeekea CCM, Mchungaji Msigwa alisema wazi na pasi na hofu, kwamba alikuwa mjinga kuwa CHADEMA. Kwa lugha rahisi, aliwatusi Watanzania wote wanaokiunga mkono Chama hicho, kwamba ni wajinga kama alivyokuwa yeye.
Sasa hebu tujiulize; leo hii Mchungaji Msigwa anataka kutuaminisha kuwa anarudi kuwa mjinga tena ndani ya CHADEMA?
Kama ndivyo, basi Mchungaji Msigwa anaingia katika historia ya kuwa miongoni mwa binadamu wachache mno duniani wanaoweza kurudi kwenye ujinga baada ya kuelimika.
Pili, najiuliza; Mchungaji Msigwa amejiridhisha kwa kiwango gani na kwa utafiti upi, kama anaweza kueleza, kwamba CHADEMA ya sasa si ya wajinga kama aliyoiacha na kutimkia (CCM)?
Tatu, Mchungaji Msigwa anaweza kutuaminisha vipi kwamba hakufuata masilahi binafsi, hasa nafasi za uteuzi, na ndiyo maana ameondoka CCM baada ya kuona amewekwa benchi na kuwa ‘mtu wa kawaida’ ndani ya Chama hicho?
Nne, kwa kuondoka kwake CHADEMA, sambamba na kauli zake za shombo, ni wazi Mchungaji Msigwa ‘alikijeruhi’ Chama, ikiwamo kukipunguzia ushawishi kwa kiasi fulani.
Kwa uandamizi wake ndani ya CHADEMA, kila baya alilosema juu ya Chama lilibeba uzito mkubwa na huenda lilibadili mitazamo ya baadhi ya wafuasi wake juu ya siasa za upinzani.
Je, Mchungaji Msigwa hajioni ni mwenye deni kubwa si tu mbele ya CHADEMA na wanachama, bali pia kwa wafuasi wake aliowaambia kuwa kushiriki siasa za upinzani ni ujinga?
Tano, Mchungaji Msigwa ameamua kujiweka katika taswira ipi kisiasa? Yule wa miaka mingi iliyopita akiwa CHADEMA, ambaye alifahamika kwa misimamo isiyoyumba, au huyu wa sasa asiyetabirika?
Mwisho, Mchungaji Msigwa ameamua kurudi CHADEMA lakini safari hii atalazimika kukubali kuwa mgeni ndani ya Chama. Kosa la kiufundi analoweza kulifanya ni kulazimisha heshima ile ile aliyokuwa nayo.
Baada ya kuondoka, kisha kukijiunga na wapinzani wakubwa, halafu kukichafua Chama, kiwango cha heshima hakiwezi kuwa kile kile. Lazima atarajie mabadiliko na akubali kuyapokea na kuishi nayo.
Hivyo, namna pekee ya kufaulu ni kukubali kuwa mgeni kwenye nyumba aliyopigania sehemu kubwa ya ujenzi wake. Kinyume chake, atatoka mchezoni. Maisha yake ndani ya Chama yatakuwa magumu mno.
Nje ya Chama, pia Mchungaji Msigwa si yule yule. Kuna picha mpya ameichora juu ya mwenendo wake wa kisiasa. Kwamba si wa kumuamini sana. Si wa kusimama naye kwa asilimia 100 ukiamini kila anachokisema. Kumbe leo atakwambia hivi, kesho atakuja na mtazamo tofauti.
Kwa maana, Mchungaji Msigwa amewapa sauti na jeuri wakosoaji wake wa ndani na nje ya Chama, ambao ni wazi wameanza kutunga mashairi ya wimbo wa ‘usaliti’ ili kuutumia kama fimbo ya kubomoa hoja na taswira yake kisiasa.
Hata hivyo, anaweza kuwajibu, kwamba yeye si mwanasiasa wa kwanza kuwa na ‘ndimi mbili’. Atawakumbusha kuhusu Wilbroad Silaha, Edward Lowassa (Mungu amrehemu) na wengineo, ambao taswira zao kwenye siasa ziliharibiwa na upepo wa kutokuaminika.


