TEHRAN, Iran
KABLA na hata wiki chache chache za mwanzoni mwa vita, Rais Donald Trump aliamini kuizima Iran na kuondosha uongozi ulioko madarakani ingechukua siku zisizozidi tatu. Aliamini ni kazi isiyohitaji matumizi ya zaidi ya saa 72.
Kinyume chake, mgogoro umeendelea kwa wiki zaidi ya saba tangu ulipoanza Februari 28, 2026, kwa Marekani na Israel kuungana kuishambulia Iran.
Katika kile kinachotafsiriwa kama kushindwa katika mpango wake, Marekani imekuja na majaribio kadhaa ya kukaa mezani na Iran ili kuona wanavyoweza kumaliza vita.
Hata hivyo, jitihada hizo zinatajwa kukwamishwa na misimamo ya kiongozi wa zamani wa jeshi aliyekuwa na cheo cha Brigedia Jenerali, Ahmad Vahidi.
ANACHORA RAMANI AKIWA MAFICHONI
Vahidi, sasa akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, hajaonekana hadharani tangu Februari 8, 2026, wiki chache kabla ya Iran kuanza kushambuliwa na vikosi vya Marekani na Israel.
Lakini, anatajwa kuwa ni mtu wa karibu wa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Mojtaba Khamenei, ambaye pia yuko mafichoni tangu aliponusurika kuuawa katika shambulizi lililomuua baba yake, Ayatollah Ali Khamenei.
Licha ya kutokujitokeza hadharani, Vahidi amekuwa akihusika katika kila hatua inayohusu mazungumzo na Marekani, ikiwa ni pamoja na kutaka vita kuendelea ikiwa Rais Trump ataona inafaa.
Vahidi aliamua kuchukua nafasi hiyo mara tu Iran na Marekani ziliposhindwa kufikia mwafaka katika mazungumzo ya kwanza yaliyofanyika Aprili, 2026 mjini Islamabad, Pakistan.
Katika mazungumzo hayo, ujumbe wa Iran uliongozwa na Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Qalibaf, aliongozana na Waziri wa Mambo ya Nje, Abbas Araghchi.
Hata hivyo, viongozi hao walikosolewa vikali mara tu waliporejea Iran, kwamba walikuwa wepesi kwenye meza ya mazungumzo. Ndipo Vahidi alipoona asimamie mwenyewe kila kitu kinachohusu mazungumzo na Marekani.
“Vahidi na watu wake karibu ndiyo wanaoamua nini kifanywe na jeshi na ndiye anayeamua pia kila kitu juu ya sera za kimataifa za Iran,” imeeleza taarifa ya Taasisi ya Masuala ya Vita ya Washington, Marekani.
YUKO TAYARI KWA LOLOTE
Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa na mshauri wa zamani wa Bunge la Marekani, Kenneth Katzman, anamtaja Vahidi kuwa ni mtu wa misimamo na aliye tayari kwa lolote juu ya uhusiano wao na Marekani.
Pia, natajwa kuwa nyuma ya mkakati wa Iran kuudhibiti Mlango-Bahari wa Hormuz, kuzuia usafirishaji wa nishati za mafuta na gesi, hatua ambayo imetikisa kwa kiwango kikubwa uchumi wa dunia.
Vilevile, Vahidi anahusishwa na mashambulizi ya Iran katika vituo vya mafuta, hoteli na miundombinu kwenye nchi za Mashariki ya Kati zenye ushirikiano na Marekani na Israel.
MAISHA, MIKASA YAKE
Jina lake halisi ni Ahmad Shahcheraghi na alizaliwa mwaka 1958 katika Miji wa Shiraz ulioko Kusini mwa Taifa la Iran. Kama ilivyokuwa kwa vijana wengi baada ya mapinduzi ya mwaka 1979, alijiunga na jeshi na kupigana vita vya miaka nane kati ya Iraq ya Saddam Hussein.
Alipanda ngazi hapo baadaye na kuanza kusimamia operesheni za nje ya nchi. Katika miaka ya 1980, alishika uongozi jeshini, ikielezwa kuwa alisimamia mfumo wa Iran kuviwezeshaji vikundi vingi vya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Ni kipindi hicho, ndipo inapoelezwa kuwa alisuka shambulizi la kigaidi katika Kituo cha Wayahudi nchini Argentina mwaka 1994 na kuua watu 85 na kujeruhi wengine 300.
Miaka miwili baadaye, chini ya uongozi wake jeshini, Iran ilitajwa kushambulia jengo la Khobar nchini Saudi Arabia na kuua watumishi 19 wa Marekani. Iran ilikana kuhusika katika mashambulizi yote mawili.
MAREKANI YAMPIGA ‘KUFULI’
Mwaka 2010, akiwa Waziri wa Ulinzi, Serikali ya Marekani ilitangaza kumuwekea vikwazo kwa madai ya kuwa sehemu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Mwaka 2022, akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alisimamia vyombo vya dola vikiua mamia ya raia walioandamana kulaani kifo cha mwenzao, Mahsa Amini, ambaye alifariki akiwa kwenye mikono ya polisi.
Baadaye, moja ya magazeti ya Iran liliripoti kwa ameagiza watumishi wa vyombo vya dola kuwafuatilia na kuwapiga picha mabinti na wanawake wasiovaa hijab nchini humo.
Licha ya kukana taarifa hizo, alishawahi kusema harakati za kuondosha uvaaji wa hijab kwa wasichana na wanawake ni mpango wa wakoloni, kwa maana ya mataifa ya Ulaya, kuharibu Dola ya Kiislam ya Iran.


