20 C
New York

Ramaphosa alivyowekwa kwenye kona kashfa ya ‘Farmgate’

Published:

PRETORIA, Afrika Kusini

KWA sasa, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini anakabiliwa na tishio la kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na rais. Amekuwa madarakani tangu mwaka 2018.

Ramaphosa, kiongozi wa zamani wa Chama cha Wachimbaji wa Madini cha Afrika Kusini, pia akitajwa miongoni mwa wafanyabiashara matajiri wa nchi hiyo, amedai kuwa hatojiuzulu, licha ya tishio hilo.

Kwa miaka nane aliyokaa madarakani, utawala wake umekuwa ukinyooshewa kidole kwa tuhuma mbalimbali za rushwa na safari hii ni kashfa ya ‘farmgate’.

CHANZO CHA TATIZO

Skendo hiyo ilianza mwaka 2020, ambapo kiasi cha Dola za Marekani 580,000 kilichokuwa kimefichwa ndani ya sofa ziliibwa, tukio lililotokea katika nyumba yake iliyoko ndani ya shamba lake la wanyama la Phala Phala.

Akisimulia tukio hilo, mkuu wa zamani wa idara ya upelelezi, Arthur Fraser, alisema Rais Ramaphosa hakuripoti polisi juu ya tukio hilo, na badala yake alifanya siri, huku akiwatumia walinzi wake kuchunguza na hata kuwakamata na kuwatesa watuhumiwa wa wizi huo.

ATOKA MAFICHONI, AKANUSHA ‘UPIGAJI’

Baada ya madai hayo, Rais Ramaphosa alitoka mafichoni na kukiri kutokea kwa wizi huo, akisema fedha hizo zilitokana na mauzo halali ya wanyama aina ya faru walioko kwenye shamba lake.

Hata hivyo, majibu hayo bado yaliacha maswali, kwamba iweje wanyama hao wabaki kwenye shamba kwa miaka zaidi ya miwili ikiwa walishauzwa?

Wakati huo, Chama chake cha ANC kilisimama naye kujaribu kumnasua kwenye skendo hiyo. Kwa wingi wa wawakilishi wake Bungeni, kilizuia kuanza kwa mchakato wa kura ya kutokuwa na imani na rais.

Ilipofika mwaka 2024, Chama cha upinzani cha mrengo wa kushoto, Economic Freedom Fighters (EFF), kinachoongozwa na kada wa zamani wa ANC, Julius Marema, kilikoleza moto upya.

Ni baada ya kuwasilisha ombi kwa Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini, kikidai kuwa Bunge lilikiuka sheria kwa kushindwa kumuwajibisha Rais Ramaphosa.

Hivi karibuni, ndipo Mahakama hiyo ilipokubaliana na hoja ya EFF, ikitaka ‘kufufuliwa’ kwa mchakato huo wa kura ya kutokuwa na imani na Rais Ramaphosa. Mwanasiasa huyo amedai atafuata sheria kupingana na uamuzi huo.

UPEPO MBAYA WA KISIASA

Kama ilivyo kwa Rais Ramaphosa sasa, mtangulizi wake, Jacob Zuma, naye hakuepuka kashfa za kujihusisha na rushwa, kiasi cha kujiuzulu mwaka 2018 akiwa hajamaliza muhula wake.

Hatua ya kujiuzulu ilitokana na Chama chake, ANC, ‘kumfungia vioo’ na kupiga kura ya kutokuwa na imani naye. Wakati wote huo wa Zuma akiongoza Chama, Ramaphosa alikuwa Naibu wake, akishika wadhifa huo tangu mwaka 2012.

Katika Uchaguzi wa mwaka 2024, baada ya awamu yake ya kwanza kumezwa na kashfa ya ‘farmgate’, ANC ilipata ushindi mwembamba zaidi kuwahi kutokea tangu mwaka 1994.

Ni kutokana na kupoteza udhibiti wake katika siasa za Afrika Kusini, ANC ililazimika kuunda serikali ya umoja kwa kushirikiana na vyama vingine vitano, kikiwamo kile kikubwa cha upinzani cha Democratic Alliance (DA).

UHUSIANO WAKE NA MAREKANI

Mbali ya kashfa za rushwa, taswira nyingine ya utawala wa Rais Ramaphosa ni uhusiano wake na Serikali ya Marekani chini ya Donald Trump.

Mara kadhaa, Rais Trump amekuwa akiiahutumu Afrika Kusini akiita kuwa ni ‘jehanamu’ kwa watu wenye ngozi nyeupe. Pia, akisema Serikali ya Rais Ramaphosa haijafanya jitihada zozote za kumaliza chagamoto hiyo.

Mei, 2025, wakati Ramaphosa alipotembelea Ikulu ya Marekani, mwenyeji wake, Trump, alimduwaza kwa kumwekea video ya mauaji ya watu weupe nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa na hata masuala ya usalama nchini Afrika Kusini, wanamkosoa Rais Trump wakisema hakuna hicho anachokiita ‘mauaji ya watu weupe’.

Wachambuzi hao wanakiri kuwapo kwa migogoro ya ardhi, lakini hawakubaliani na hoja kwamba watu weupe ndiyo wahanga wakubwa katika hilo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img