WASHINGTON, Marekani
JARIDA la Wall Street Journal linaripoti kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump, amewaambia wasaidizi wake kuwa yuko tayari kusitisha operesheni ya kijeshi dhidi ya Iran hata kama Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kufungwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, maafisa wa utawala wa Marekani wamesema kuwa Trump na timu yake walikuwa na wasiwasi kuwa kutumia nguvu za kijeshi kufungua njia hiyo muhimu ya usafirishaji wa mafuta kunaweza kuurefusha mzozo huo zaidi ya muda uliokadiriwa wa wiki nne hadi sita.
Badala yake, kiongozi huyo anaripotiwa kuelekeza mkakati wa kupunguza makali ya mapigano, baada ya kile kinachoelezwa kuwa ni uharibifu mkubwa kwa jeshi la wanamaji la Iran pamoja na hifadhi yake ya makombora.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Trump anaweza kuelekeza nguvu zaidi katika njia za kidiplomasia ili kuishinikiza Iran kufungua tena Mlango wa Hormuz, ambao ni muhimu kwa biashara ya kimataifa.
Hata hivyo, msimamo huo bado haujathibitishwa rasmi, ambapo Shirika la Habari la BBC limesema limewasiliana na Ikulu ya White House kwa maoni.
Iwapo taarifa hiyo itathibitishwa, inaweza kuashiria mabadiliko ya mkakati wa Marekani kutoka hatua za kijeshi kwenda diplomasia katika kukabiliana na mvutano unaoendelea katika eneo la Ghuba.


