PARIS, Ufaransa
INAELEZWA kuwa Zinedine Zidane ‘Zizou’ amefikia makubaliano ya kuinoa timu ya taifa ya Ufaransa na ataanza kazi hiyo baada ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Kwamba kocha wa sasa, Didier Deschamps, amebakiza michuano hiyo tu kabla ya kumpisha mkongwe mwenzake huyo.
Deschamps (56), amekuwa kwenye benchi la ufundi la ‘Le Bleus’ na sehemu ya mafanikio yake ni kuipa ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2018.
Katika michuano iliyopita nchini Qatar, aliifikisha fainali, na kisha kutangaza kuwa ataondoka baada ya hizi za mwaka huu zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico.
Zidane (53), kwa upande wake, amekuwa nje ya kazi ya ukocha tangu alipoachana na Real Madrid mwaka 2021.
Ripoti zinaeleza kuwa ‘Zizou’ amekataa ofa nyingi ili kutimiza ndoto yake ya kuliongoza benchi la ufundi la timu ya taifa ya Ufaransa.
Licha ya kwamba hana uzoefu katika ngazi ya timu ya taifa, Zidane ni miongoni mwa makocha mwenye mafanikio makubwa, akikumbukwa kwa mataji matatu mfululizo na mawili ya La Liga akiwa Santiago Bernabeu.
Mbali ya mafanikio hayo, anakutana na kikosi cha Ufaransa kilichojaa wachezaji wa viwango vya juu, wakiwamo Kylian Mbappe, Ousmane Dembele, Michael Olise, Rayan Cherki na Warren Zaire-Emery.


