6.5 C
New York

Unabeti kama starehe au na wewe umeshaigeuza ajira?

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

SHIDA kubwa tuliyonayo ngozi nyeusi ni kushindwa kutofautisha kati ya jambo la starehe na lile la lazima/muhimu. Hao ndipo tunapofeli.

Huwa tunaanza kama starehe, kisha tunalowea huko na kuwa sehemu muhimu ya maisha. Tukifika huko, tunakuwa taabani na hatuwezi tena kujinasua.

Hebu tuanzie mbali kidogo. Jiulize; kama tunakubaliana kuwa pombe ni starehe, inawezekana vipi mtu aamkie, ashinde na alale baa?

Tujiulize tena; inawezekana vipi mtu anywe pombe kila siku? Huyo kwake pombe ni starehe au imeshakuwa ‘wajibu’?

Kijana anayeanza kuvuta sigara akiamini ni starehe yake, ataanza na moja au mbili kwa siku. Tena akivuta asubuhi, nyingine atavuta jioni au usiku.

Baada ya mwezi, utakuta anavuta pakti moja kwa siku. Tafsiri yake ni nini? Sigara imeshakuwa wajibu kwake. Siyo tena starehe.

Sasa iko hivi; kubeti ilianza kama ambavyo nimejaribu kugusia kwenye pombe na sigara. Ilikuwa ni starehe, ambayo haikuhusishwa kabisa na ajira.

Vijana wangeweza kubeti na kuendelea na ‘mitikasi’ yao ya kila siku ya kujiingizia kipato. Kubeti ilikuwa starehe tu.

Kwa kadiri vijana walivyojiingiza na kufahamu mchezo huo, taratibu wakajijuta wanalowea huko na sasa wameufanya kuwa ajira na jambo muhimu kwao.

Kwamba si ajabu sasa kukuta vijana wamejirundika kwenye mabanda ya kubeti kuanzia asubuhi, mchana hadi jioni.

Ukiuliza kazi wamefanya muda gani, unajijibu kuwa tayari kwao kubeti imeshakuwa ajira na njia kuu ya kupata kipato. Ni hatari!

Kwamba kama ilivyo kubeti, ambapo tunakubaliana kuwa ni mchezo wa ‘pata potea’, kijana naye ameamua kuyafanya maisha yake kuwa ni ya bahati nasibu.

Kwa ufupi, kesho yake itategemea matokeo ya mechi kati ya Manchester United na Chelsa, pia Arsenal ishinde kuanzia mabao mawili, wakati huo huo Bayern Munich imalize dakika 90 bila kuruhusu bao. Ajabu sana!

Sikatai, wapo wanaopata fedha, tena nyingi tu kupitia kubeti. Lakini tujiulize; ni wangapi kati ya wengi tunaokutana nao wakijisonya baada ya kuchana mikeka?

Ni wangapi tunaowafahamu kwa sura, ambao tumeona kwa sasa ni matajiri kupitia kubeti? Wapo, lakini ni wachache, ukilinganisha na ‘wanaopasuka’.

Sasa, utakuwa na wendawazimu kiasi gani kuweka hatima yako ya maisha katika biashara ya aina hiyo? Ambayo haikupi mifano halisi ya waliotoboa?

Binafsi, nimegoma. Kesho yangu siwezi kuikabidhi kwa Bayern Munich. Siwezi kuacha hatima ya familia yangu isubiri matokeo ya Liverpool. Sitaki!

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img