6.5 C
New York

Kanisa Katoliki Tanzania na historia ya majina ya maaskofu wake

Published:

Na Malisa GJ

KATIKA historia ya Kanisa Katoliki nchini Tanzania kumekuwa na Maaskofu Wakuu watatu (Archbishops) wenye jina Rugambwa. Wawili kati yao wakiwa Makardinali na mmoja Balozi wa Papa.

Wa kwanza ni Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam na Kardinali wa kwanza Mwafrika.

Wa pili ni Mhashamu Askofu Mkuu Novatus Rugambwa, aliyekuwa Balozi wa Papa nchini New Zealand na wa tatu ni Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Tabora.

Kwa haraka ukisikia majina haya utadhani huenda ni ndugu au watu wanaotoka ukoo mmoja. Lakini si ndugu kabisa.

Kimsingi mwenye ukoo wa Rugambwa ni mmoja, Laurean Kardinali Rugambwa. Hao wengine walivutwa na utume wa Kardinali Rugambwa “wakakopa” jina.

Tuanze na Laurean Rugambwa mwenye jina lake. Alizaliwa 12/07/1912 huko Bukoba. Mwaka 1943 akapata daraja takatifu la Upadre.

Mwaka 1949 alihitimu masomo yake ya shahada ya udaktari wa sheria kutoka Chuo Kikuu cha Urbaniana, Roma. Mwaka 1951 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Febiana (Titular Bishop).

Mwaka 1953 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Rutabo (leo linajulikana kama Bukoba). Mwaka 1960 akateuliwa kuwa Kardinali, na kuweka rekodi ya kuwa Mwafrika wa kwanza kusini mwa Sahara kuwa Kardinali.

Mwaka 1968 akateuliwa na Papa Paul VI kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam.

Akatumikia Jimbo Kuu Dar es Salaam kwa miaka 24 hadi mwaka 1992 alipostaafu. Mwaka 1997 alifariki akiwa na miaka 86 na kuzikwa Jimboni Bukoba.

Wa pili ni Askofu Mkuu, Novatus Rugambwa. Huyu si Rugambwa. Alizaliwa tarehe 08/10/1957 akiitwa Novatus Benedict Rwechungura.

Wakati ule Askofu Rugambwa alikuwa anaongoza Jimbo Katoliki Rutabo (kwa sasa Bukoba). Wazazi wa Novatus walivutiwa sana na utume wa Askofu Rugambwa.

Mwaka 1958 wakati wanambatiza mtoto wao wakampa jina Novatus Rugambwa, wakimtakia matashi mema ili naye aje kuwa Askofu.

Ama kweli maneno yanaumba. Novatus akapata wito wa Upadre. Mwaka 1986 akapata daraja takatifu la Upadre. Baadaye akatumwa masomoni Chuo Kikuu cha Urbaniana, Roma na kuhitimu shahada ya udaktari wa sheria mwaka 1991.

Mwaka 2010 akateuliwa kuwa Askofu Mkuu na Balozi wa Papa huko São Tomé na Príncipe. Baadaye akahamishiwa Angola, kisha Honduras na hatimaye New Zealand.

Alifariki Septemba 16, 2025 huko Roma baada ya kuugua na kupooza kwa miaka miwili. Akazikwa tarehe 29 Septemba 2025, Jimboni Bukoba.

Kwa hiyo ndani ya Kanisa Kuu (Cathedral) la Jimbo Katoliki Bukoba wamezikwa Maaskofu watatu. Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, Mhashamu Nestory Timanywa na Mhashamu Novatus Rugambwa.

Wa tatu ni Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa. Huyu naye si Rugambwa. Alipozaliwa aliitwa Protase Abakaraza, ilikua Mei 31, mwaka 1960.

Siku chache kabla hajazaliwa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa alikua ametembelea Parokia ya Bunena (kijiji alichozaliwa Protase).

Wakati wa kubatizwa ulipowadia, Mjomba wake alipendekeza aitwe Rugambwa. Hii ni kwa sababu alikua rafiki sana na Kardinali Rugambwa, na pia Kardinali Rugambwa alitembelea parokia yao siku chache kabla ya kuzaliwa kwake.

Hivyo akaitwa Protase Rugambwa, kumtakia matashi mema ya kuwa kama Kardinali Laurean Rugambwa.

Maneno yanaumba bwana. Protase akapata wito wa Upadre na baada ya kusoma shahada ya Falsafa na Theolojia, hatimaye mwaka 1990 akapata daraja takatifu la Upadre.

Akafanya kazi mbalimbali za kitume, na mwaka 1994 akatumwa masomoni Chuo Kikuu Lateran. Mwaka 1998 akahitimu shahada ya udaktari katika theolojia ya uchungaji.

Mwaka 2008 akateuliwa na Papa Benedict XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma. Tarehe 26 Juni 2012 akateuliwa kuwa Katibu Msaidizi Mkuu wa Baraza la Uinjilishaji.

Akatoka Kigoma akahamia Vatican. Mwaka 2017 akapandishwa kuwa Katibu Mkuu wa baraza hilo, na akateuliwa pia kuwa Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari.

Ili kutimiza majukumu yake ipasavyo akateuliwa kuwa Askofu Mkuu (Archbishop).

Akatumikia wadhifa huo hadi Aprili 13, 2023 alipoteuliwa kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi wa Jimbo Kuu Tabora kuchukua nafasi ya Askofu Mkuu, Mhashamu Paul Ruzoka ambaye aliomba kustaafu.

Julai 9, 2023 Papa Francis akamteua kuwa Kardinali. Akawa Kardinali wa 3 nchini baada ya Laurean Kardinali Rugambwa, Polycarp Kardinali Pengo na yeye Protase Kardinali Rugambwa.

Umeona jina linavyobeba tabia? Biblia inasema: “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi, na neema kuliko fedha na dhahabu” (Mithali 22:1).

Wazazi wa Novatus Rwechungura walitamani mtoto wao awe Askofu kama Rugambwa, wakambadili jina kutoka Novatus Rwechungura kuwa Novatus Rugambwa. Na akawa Askofu.

Wazazi wa Protase Abakaraza walifurahi mtoto wao alipozaliwa siku ambayo Kardinali Rugambwa aliwatembelea. Wakambadili jina kutoka Protase Abakaraza kuwa Protase Rugambwa wakimuombea matashi mema aje kuwa Kardinali. Na amekuwa.

Je wewe Ngengemkeni Mitomingi unawapa watoto wako majina gani? Unamwita mwanao Kibakuli halafu unataka aje kuwa Meneja wa benki? Yaani tukabidhi pesa zetu kwa Kibakuli? Kumbuka maandiko yanasema heri jina jema kuliko mali nyingi, na heri neema kuliko fedha na dhahabu.!

Mwandishi wa makala haya ni mchambuzi mbobevu wa masuala ya kijamii na kisiasa.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img