PARIS, Ufaransa
KOCHA wa PSG raia wa Hispania, Luis Enrique, havutiwi na mpango wa kuinoa Manchester United, licha ya kuhusishwa na klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.
Taarifa zilizopo zinadai kuwa mabosi wa Man United walifunga safari hadi jijini Paris kumfuata Enrique ili kumshawishi atue Old Trafford.
Hata hivyo, kocha huyo haonekani kuitaka ofa yao, na badala yake anatamani kuendelea kuliongoza benchi la ufundi la PSG.
Mkataba wake na matajiri hao wa Ligue 1 unatarajiwa kufikia ukomo mwishoni mwa msimu ujao (2026-27).
Wakati huo huo, inaelezwa kuwa tayari Enrique ameshakaa mezani na Mkurugenzi wa Michezo wa PSG, Luis Campos, kujadili ‘ishu’ ya mkataba mpya utakaofikia ukomo mwaka 2030.
Kwa sasa, Michael Carrick ndiye anayeinoa Man United lakini mabosi wa Old Trafford wanaamini kiungo wao huyo wa zamani hana uzoefu wa kutosha.


