Na mwandishi wetu, Gazetini
HISTORIA ya maisha ya Bob Nesta Marley ina mengi ya kusisimua, ikiwa ni safari iliyoanzia Februari 6, 1945 na kufikia tamati yake Mei 11, 1981.
Kwa kipindi hicho cha miaka 36 aliyojaaliwa kuishi katika uso wa dunia, Bob ameacha si tu jina, bali pia heshima na mafanikio makubwa kupitia sanaa ya muziki wa Reggae.
Leo hii, jina lake limebaki kuwa alama ya Reggae, akiitoa kutoka muziki wa Jamaica na kuupa nafasi katika jukwaa la kimataifa na dunia kwa ujumla.
GAZETINI kupitia vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa inakuletea mfululizo wa makala ya maisha ya gwiji huyo, ikigusia kuzaliwa kwake, changamoto na mafanikio yake kwenye jukwaa la muziki.
Katika sehemu ya kwanza ya makala haya yatakayokujia kila Jumamosi, tunaangazia kuzaliwa kwake, kwa maana ya safari yake kabla ya kuwa maarufu. Karibu.
Bob, kama nilivyoeleza awali, alizaliwa Februari 6, 1945 mjini Nine Mile nchini Jamaica. Baba yake mzazi ni Norval Sinclair Marley na mama anaitwa Cedella Malcolm.
Historia inatumbukusha kuwa Norval alikuwa ni chotara wa Jamaica mwenye asili ya Visiwa vya Wales, Uingereza.

Hata hivyo, baadhi ya vyanzo vinaeleza kuwa Norval alikuwa na asili ya Syria na Israel, ingawa wapo wanaokanusha na kusema alikuwa na asili ya Wales tu.
Alikutana vipi na Cedella? Norval alikuwa mtumishi wa jeshi la Uingereza, hivyo uwepo wake nchini Jamaica ulikuwa ni kwa ajili ya kusimamia mradi wa ugawaji wa ardhi.
Katika harakati hizo, akakutana na mrembo (Cedella), ambaye wakati huo alikuwa binti mwenye umri wa miaka 18 tu.
Vyanzo vinadai kuwa Norval alikuwa na umri wa miaka 64 wakati Bob anazaliwa lakini alishindwa kumuoa Cedella kutokana na familia yake.
Ndiyo, familia yake haikutaka kuona Norval, ambaye ni mzungu, anamuoa mwanamke mwenye ngozi nyeusi, achilia mbali anayetoka Jamaica.
Licha ya kushindwa kumuoa Cedella, bado Norval aliendeleza ukaribu naye, ikiwa ni pamoja na kutuma fedha za matumizi hata aliporejea Uingereza. Mbaya zaidi, Norval alifariki wakati ndiyo kwanza Bob ana umri wa miaka 12.
Ndipo Bob na mama yake walipoamua kuondoka Nine Mile na kuhamia mji mwingine. Wakahamia Kingston, Mji Mkuu wa Jamaica.
Wakiwa Kingston, Cedella alikutana na mwanaume mwingine. Safari hii, alikuwa ni Thadeus Livingston.
Kama ilivyo kwa Cedella, Thadeus naye alikuwa ‘singo’, ingawa tayari alikuwa na mtoto wa kiume aitwaye Neville Livingsto ‘Bunny Wailer’.
Ukaribu wa Cedella na Thadeus si tu uliwapatia binti aitwaye Claudette Pearl, bali pia ulisababisha Bob na Bunny kuishi pamoja na hata kusoma shule moja.
Wakiwa nyumbani na hata shule, Bob na Bunny walionesha vipaji vikubwa vya muziki, wakijaribu kuimba kwa kukopi kazi za wasanii wakubwa wa R&B wa Marekani.
Kwa leo, makala haya ya simulizi ya maisha na mikasa ya Bob Nesta Marley itaishia hapa. Kwa mwendelezo, tukutane hapa Jumamosi ya wiki ijayo.
Itaendelea kwa maoni, ushauri +255 744 187 871


