6.5 C
New York

Tanzania yajipanga kuwa kitovu cha uwekezaji wa madini Afrika

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kujiimarisha kama kitovu cha uwekezaji wa kimkakati barani Afrika, Serikali kupitia Wizara ya Madini imekaribisha kampuni kutoka Korea Kusini kuja kuwekeza nchini, ikieleza kuwepo kwa fursa lukuki katika utafiti wa madini, uongezaji thamani pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa za uchimbaji na uchakataji wa madini, hususan madini muhimu na ya kimkakati.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, ameyasema hayo Januari 28, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza na ujumbe kutoka Korea Kusini uliowajumuisha wawakilishi wa Shirika la Kukuza Biashara na Uwekezaji la Jamhuri ya Korea (KOTRA) pamoja na Kampuni ya HD Construction Equipment, inayojihusisha na utengenezaji wa vifaa na teknolojia za uchimbaji na viwanda.

Mbibo amesema sera na maboresho ya kisheria yaliyofanywa na Serikali katika sekta ya madini yamelenga kuvutia mitaji yenye teknolojia ya kisasa, ujuzi wa kitaalamu na mtazamo wa uwekezaji wa muda mrefu, hususan katika uchakataji wa madini ndani ya nchi, ujenzi wa viwanda na uhamishaji wa teknolojia.

“Tanzania iko tayari kwa ubia wa kimkakati unaoongeza ajira, mapato ya ndani na ushindani wa kimataifa. Tunakaribisha wawekezaji wanaoleta suluhisho za kisasa katika mnyororo mzima wa thamani wa madini, kuanzia utafiti hadi uongezaji thamani ndani ya nchi, hususan kwa madini muhimu na mkakati,” amesema Mbibo.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi na Kamishna wa Biashara wa KOTRA, Ofisi ya Dar es Salaam, Kim Sangwoo, amesema Korea Kusini ina nia ya kuongeza uwekezaji wake katika Ukanda wa Afrika Mashariki kupitia miradi yenye tija, uwajibikaji na manufaa ya pande zote, huku Tanzania ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye mazingira bora ya uwekezaji.

Naye Meneja Mkuu wa Kampuni ya HD Construction Equipment, Soohong Min, amesema kampuni za Korea zina uzoefu mkubwa katika teknolojia za uchimbaji, vifaa vizito vya kisasa na mifumo ya uzalishaji yenye ufanisi, uwezo ambao unaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuharakisha ajenda ya Tanzania ya uongezaji thamani wa madini.

Majadiliano hayo yalihusisha maeneo mbalimbali muhimu yakiwemo utafiti wa kina wa madini kwa kutumia teknolojia za kisasa, uchakataji na uongezaji thamani, ujenzi wa viwanda na miundombinu ya uzalishaji pamoja na uhamishaji wa teknolojia kwa wataalamu wa ndani.

Kwa kuhitimisha, pande zote zimeonesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiteknolojia, huku Tanzania ikiweka wazi kuwa mlango uko wazi kwa wawekezaji wanaoendana na dira ya maendeleo jumuishi na endelevu kwa manufaa ya kiuchumi, teknolojia na kijamii.

KOTRA ni shirika la Serikali ya Korea Kusini lililoanzishwa mwaka 1962 kwa lengo la kuhimiza biashara ya kimataifa na uwekezaji wa kigeni, likiwa na ofisi katika nchi mbalimbali duniani, ikiwemo Dar es Salaam.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img