9.2 C
New York

Visual| A-Z yaliyojiri fainali za AFCON 2025

Published:

RABAT, Morocco

BAO pekee la staa wa Villarreal ya Hispania, Pape Gueye, limehitimisha msimu huu wa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) kwa kuipa ubingwa Senegal katika mchezo wao dhidi ya wenyeji Morocco.

Senegal wamebeba taji hilo, ikiwa ni miaka minne pekee imepita tangu walipokuwa mabingwa wa AFCON mwaka 2021.

Je, ni yapi yaliyojiri na kuwa gumzo kwa kipindi chote cha mwezi mmoja wa mashindano hayo yaliyoanza Desemba 31, 2025? Makala haya yanachambua.

Algeria yavunja mwiko

Kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019, timu ya taifa ya Algeria ilifanikiwa kuvuka makundi na kuingia hatua ya mtoano (16 Bora) ya fainali za AFCON.

Hata hivyo, baada ya kuifunga DRC katika mchezo wa 16 Bora, safari yao ilikwamia robo fainali, ambapo walifungwa na Nigeria ‘Super Eagles’.

Kocha azinguana na Waziri

Ni kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’, Hugo Broos, ambaye alitibuana na Waziri wa Michezo, Gayton McKenzie.

Walitofautiana baada ya Broos kusema fainali za AFCON zilizofanyika Morocco hazikuwa na mvuto, ukilinganisha na zile zilizopita nchini Ivory Coast.

Misri yaendeleza ‘uteja’ kwa Senegal

Mabingwa mara nyingi (7) wa fainali za AFCON, Misri, waliishia nusu fainali baada ya kufungwa bao 1-0 na Senegal ‘Simba wa Teranga’.

Kwa mujibu wa rekodi, hicho kilikuwa ni kipigo cha tatu mfululizo kwa Misri mbele ya vigogo hao wa soka la Afrika ya Magharibi.

Mabingwa watetezi mapema tu

Msimu uliopita wa fainali za AFCON, 2024, timu ya taifa ya Ivory Coast ndiyo iliyofanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

Safari hii, mambo yalikuwa magumu kwa vijana hao wa kocha Emerse Fae kwani waliishia robo fainali, wakiondoshwa na ‘Mafarao’ wa Misri.

Mastaa wa Ulaya wapondwa

Baada ya Misri kupoteza mchezo wa kusaka mshindi wa tatu dhidi ya Nigeria, mkongwe wao, Wael Gomaa, aliibuka.

Gomaa alimtaka kocha Hossam Hassan kuacha kuwaita wachezaji wanaocheza Ulaya akisema hawana mchango wowote kikosini.

Rekodi ya mvua ya mabao

Zikikuwa ni fainali za mabao mengi. Kwa kipindi chote cha mashindano hayo, nyavu zilitikiswa mara 121, idadi ambayo ni mara mbili ya yale ya msimu uliopita (2024).

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Morocco anayekipiga Ulaya akiwa na Real Madrid, Brahim Diaz, ndiye aliyeibuka mfungaji bora kwa mabao matano.

Mali na mkosi wa kadi nyekundu

Katika mechi tatu mfululizo, timu ya taifa ya Mali ‘Eagles’ ililazimika kumaliza ikiwa na wachezaji 10 uwanjani.

Amadou Haidara, Woyo Coulibaly na nahodha wao, Yves Bissouma, walikumbana na ‘umeme’ katika matukio tofauti.

Michuano ilikosa ‘hat-trick’

Licha ya fainali za AFCON 2025 kushuhudia mabao mengi yakifungwa, hakuna mchezaji aliyeondoka Morocco akiwa na amefunga mara tatu katika mchezo mmoja (hat-trick).

Nicolas Jackson wa Ivory Coast, alikuwa mchezaji wa kwanza msimu huu wa AFCON kufunga mabao mawili ya mchezo mmoja.

Nigeria wakali wa mshindi wa tatu

Mshambuliaji wa Atalanta ya Serie A, Ademola Lookman, alifunga penalti ya ushindi iliyopa Nigeria ushindi katika mchezo dhidi ya Misri uliokuwa wa kusaka mshindi wa tatu.

Hiyo ikawa ni kwa mara ya nane kuiona Super Eagles ikishinda mechi zake za kusaka mshindi wa tatu katika historia ya AFCON. Pia, ndiyo timu iliyofunga mabao mengi (14) msimu huu.

Wakali wa kujifunga

Katika mashindano ya AFCON msimu huu, wachezaji wanne wa timu tofauti walikumbana na balaa la kujifunga.

Nyota hao ni Ahmed Fatouh (Misri), Saul Coco (Guinea ya Ikweta), Feliciano ‘Nene’ Jone (Msumbiji) na Aubrey Modiba (Afrika Kusini).

Mchezaji ‘mzee’ zaidi astaafu

Katika fainali za msimu huu, kiungo wa Msumbiji, Elias Pelembe, alikuwa ndiye mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi (miaka 42).

Hata hivyo, Pelembe ameshatangaza kustaafu. Ni mchezaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi kucheza AFCON baada ya Essam El Hadary wa Misri.

Tanzania yaacha rekodi

Kwa mara ya kwanza katika historia ya AFCON, timu ya soka ya taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’, ilivuka hatua ya makundi.

Wangeweza kuvuka hata hatua ya 16 Bora kama si kufungwa bao 1-0 na wenyeji wa michuano hiyo, Morocco ‘Simba wa Atlas’.

Uganda yatumia makipa watatu

Timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ imekuwa ya kwanza katika historia ya AFCON kutumia makipa watatu kwenye mechi moja.

Katika mchezo dhidi ya Nigeria, walianza na kipa Denis Onyango lakini aliumia. Akaingia Salim Magoola, ambaye hata hivyo alilimwa kadi nyekundu na kumpisha Nathan Alionzi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img