3.7 C
New York

Enyi Watanganyika, ni nani aliyewaroga?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

KELELE za kukera, kama si za kuchefu kabisa, zinakita kwenye ngoma za masikio yangu. Kelele zinazojirudia, zinazochefua na kunipa picha ya matapishi. Kero!

Ni kelele ambazo nilizoea kuzisikia kwa majirani zetu. Siyo ndani ya nchi hii. Siyo katika ardhi hii ya Tanganyika (Bara) wala kwa ndugu zetu wa Zanzibar.
Labda Kenya au Uganda. Huko nilizisikia kwa miaka mingi. Nilishazizoea na hazikuwa zikiniumiza. Labda ni kutokana na umbali.

Kwa Tanganyika na Zanzibar, kelele hizi ni mpya. Kutokana na ugeni na ukaribu wake, mwangwi wa sauti ya kelele hizo unaumiza na kuyapa wakati mgumu masikio yangu. Sijui cha kufanya, ila zinakera mno!

Sidhani kama niko peke yangu katika hili. Naamini, pasi na chembe ya shaka, wapo wengi wanaokerwa na kelele hizo. Labda hawana pa kusemea na wamebaki na manung’uniko tu.

Mbaya zaidi, ni ngumu kuepuka kufikiwa na sauti ya kelele hizo. Zilianzia mitandaoni na sasa zimefika hata kwenye mijadala ya vijiweni, ambako tulizoea kukuta utani wa soka na siasa kwa mbali.

Enyi Watanganyika, pamoja na ndugu zenu Wazanzibar, ni nani aliyewaroga na kujikuta mkikubali kuzipa nafasi kelele zinazoumiza masikio yetu?
Ni nani aliyegeuka kirusi cha kubeba kelele hizo kutoka huko tulikozoea kuzisikia na kuzileta katika ardhi yenu?

Bado najiuliza kwa tafakuri; huyo aliyezibeba ana maana gani? Ametumwa au amejituma? Itakuwaje endapo atafanikiwa zaidi ya hapa?

Tujikumbushe; kwa miaka mingi tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane na ‘kuizaa’ Tanzania mwaka 1964, hatukuwahi kugawanyika kwa misingi ya tofauti za imani zetu za dini.
Tunaweza kuwa tulitofautiana mara kadhaa kimtazamo, lakini bado tofauti ya dini haikuwahi kufanikiwa kujenga ukuta kati ya Muislamu, Mkristo na Mpagani.

Kipimo cha ukomavu wetu wa kuheshimiana na kuvumiliana katika misingi ya dini ni mikutano ya hadhara ya wakati ule, ambayo ilihusisha ‘minyukano’ ya hoja kati ya wanazuoni wa Kiislamu na ndugu zao Wakristo.
Mwisho wa siku, Muislamu alibaki na mafundisho yake na Mkristo akabeba Biblia yake na kile alichokiamini. Tulibaki kama familia inayoishi vyumba tofauti ndani ya nyumba moja.

Zilipotokea tofauti zilizoashiria mpasuko, jamii kwa pamoja ilibeba dhima ya kukishughulikia kirusi hicho ili kila Mtanganyika na Mzanzibar awe huru kwa kile anachokiamini.
Katika jamii ya Watanganyika na Wazanzibar, hakukuwa na dini iliyo bora kuliko nyingine, bali ubora wake utabaki kwa yule anayeiamini na kuifuata tu. Si vinginevyo.

Leo hii, ni nani aliyewaroga Watanganyika na Wazanzibar? Msingi wa swali hilo ni kile kinachoendelea mitandaoni na vijiweni, ambako imekuwapo mijadala inayoshinikiza mpasuko kati ya waumini wa Uislamu na Ukristo.

Haishangazi tena kuona baadhi ya waumini, wengine wakifahamika kwa elimu kubwa ya dini, kuja na kauli za kukejeli imani za dini za wenzao. Ni kawaida tu!
Wakati huo huo, kelele hizo za kukera zimekuwa zikileta mpasuko hata kwa waumini wa dini moja, wakishambuliana kwa kuwa tu wanatokea madhehebu tofauti.

Swali ni je; tofauti ya dini au dhehebu inatosha kutugawa kama jamii? Ikiwa tumekubali mpasuko huo, ipi hatima yetu mbele ya ‘maadui’ zetu wa nje?

Mwisho; tunaweza kukubali kutokukubaliana katika misingi ya dini. Kwamba kama umechagua kuwa Muislamu, basi zipo sababu za msingi zilizonisukuma kuchagua Ukristo.
Tukiishia hapo, tutafanikiwa kuepuka mtego wa kutugawa na kutunyima haki ya kuwa familia yenye upendo, inayoishi vyumba tofauti ndani ya nyumba moja.

Niishie hapo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img